Nuru Ndani Yako

Nuru Ndani Yako
Nuru Ndani Yako
Subscribe For Free Updates!

We'll not spam mate! We promise.

KARIBU SANA

HONGERA KWA KUCHAGUA BLOG HII.MAISHA NI UCHAGUZI...NA KILA UCHAGUZI NI SAHIHI....KILA UCHAGUZI UNA MATOKEO YAKE.......KUCHAGUA KUSOMA YALIYO KATIKA BLOG HII KUTAKUFANYA UJITAMBUE,,UUJUE UWEZO MKUBWA ULIO NDANI MWAKO NA HIVYO KUFIKIA MAFANIKIO UNAYOYAKUSUDIA........WEWE NI ZAIDI YA UJIONAVYO,NI ZAIDI YA UJIPIMIAVYO.....UTATAMBUA YA KUWA MUNGU AMBAYE KILA UCHAO WATU WANAMTAFUTA...YU NDANI MWAKO.....UTATAMBUA KUWA U MWANGAZA.....NA UTATAMBUA JINSI YA KUUTUMIA KUWAMULIKA WENGINE...NA KUIFANYA NURU YA MUNGU ILIYO NDANI MWAKO IONEKANA KWA WENGINE-PONGU JOSEPH
Showing posts with label TEACHINGS OF THE WISE. Show all posts
Showing posts with label TEACHINGS OF THE WISE. Show all posts

Monday, September 30

SIFA ZA BINADAMU ANAYEJITAMBUA

Katika makala hii tunajifunza juu ya binadamu anayejitambua.Makala hii inaweza kukukumbusha mambo mengi kwa kifupi na hivyo kukufanya uchunguze juu ya maisha yako na kuyatumia vyema kwa wakati huu ulipo hapa duniani.


Kutambua ndani yako hakuhitaji uende shule na kusoma sana,na hakutokani na maamuzi ya mtu mwingine bali ni maamuzi yatokayo ndani mwako
Ni mguso unaotaka ndani mwako, ufahamu unaokua toka ndani mwako. Ni uchimbuzi wa chemchem zitokazo ndani mwako, Ni kumtambua Mungu kupitia mguso ndani ya moyo wako, kisha kuanza kutumia kipawa ulichonacho kwa ajili ya utukufu  wa Mungu . Ni hisia za ndani zitakazofanya umfahamu Mungu na si kufikiria tu.Upya ndani ya binadamu hutokea wakati wote  kwa kuunganisha moyo wako na ulimwengu wa hisia na kuendelea kujifunza kila wakati na kukuza nafasi ya moyo wako kuwa mpya.
 na
Je ni kwa namna gani unamtambua binadamu anayejitambua?

Mtu anayejitambua hubadili mtazamo wake kutoka kwenye mtazamo wa jamii unaofuata mila na desturi/kawaida kuelekea kwenye fikra za kuijenga dunia mpya na yenye fursa mpya.Hujenga dunia ambayo wanaomzunguka ni wanadamu wanaotambua utu na nafasi ya kila nafsi.Akiwa na misingi ya ujamaa na usawa, hufanya majukumu yake kutoka kujitazama yeye binafsi na kuanza kuwatazama wengine.Uchaguzi wake na matendo yake husukumwa na  maono na mtazamo wa mbali kwa ajili ya binadamu wote na viumbe vyote.Hutazama sio kila kiumbe kwa ajili yake,bali kila kiumbe kwa ajili ya wote.

Anayejitambua habagui jinsia bali hutambua jinsia kuwa ni matokeo ya fikra za Mungu yaliyokusuduia kutoa fursa.Huheshimu, hutambua wengine na kuthamini nafsi zao na uchaguzi wao.Hutengeneza dunia dunia ambayo jinsia zote huwa na uhuru wa  kutumia vipawa vyao, kutambua sauti zo,nuru ndani mwao na kutumia kwa ajili ya viumbe wote. 

Mtu anayejitambua hasukumwi kutenda na maamuzi ama fikra za wengine. Anatazama ndani yake.Hajifananishi na nafsi zingine na hivyo hatumii nafasi yeyote kuwakandamiza wengine.Husimama kwa miguu yake mwenyewe. Anawasikiliza wengine isipokuwa hatoi nafasi kwa wengine kumuamulia maisha atakayoishi. Anayaona mambo yajayo na hivyo huanza kuijenga kesho yake katika wakati tunaouita sasa. Ni alama ya uwezo wa Mungu uliopo ndani ya binadamu. Na alama ya maisha yake huishi enzi na enzi.

Mtu anayejitambua huchukua hatua juu ya hisia zitokazo ndani mwake na hivyo kutambua matokeo ya matendo yake.Hutenda kwa msukumo wa moyo. Hutambua mambo ambayo hayamletei faida na kutoyafanya na pia hutambua yale yanayomletea faida ..akitambua kuwa anapotenda kwa wengine anajitendea mwenyewe. Husikiliza hisia za ndani mwake na kujifunza lugha ya moyo wake.

Huishi maisha yenye sababu. Husikia muito alioitiwa na kuuuishi. Haridhishwi tu na maisha ya tokanayo na matukio kama kuamka,kutembea,kulala,kula bali hutambua kuwa yupo hapa duniani kwa sababu maalum,hivyo huchimba ndani mwake kuijua sababu na kuiiishi. Kila wakati anasukumwa na sababu hiyo  ya yeye kuishi ,kuendelea kuishi kwa dhati akitengeneza na  kuifuata njia inayomfikisha huko.

Hakimbii majukumu yake . Hajitoi katika kutafuta suluhu ya changamoto na wala halaumu wengine. Hutambua makosa yake na kujifunza kupitia hayo. Husanifu maisha yake na kuyafanya mapya kila wakati.
Hujifunza toka ndani mwake na kutoka kwa wengine. Hutilia mkazo katika mafanikio ya ukuaji ndani mwake kuliko mafanikio ya nje., hutengeneza ndani mwake. Hutafiti na kuvumbua chemchem zinazojenga na kubomoa nafsi na kutumia chemchem hiyo kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi.Hivyo aliyejitambua ni picha tosha ya uwezo na uwepo wa Mungu ndani ya binadamu. Hutengeneza msawazo kati ya chemchem ndani mwake na matokeo yaonekanayo halisia.;
Binadamu anayejitambua hutazama kila jambo kama fursa


Anayejitambua hatafuti usahihi katika utendaji bali hutenda kwa kujitolea katika nguvu na uwezo wote.Hufanya kwa uwezo wake wote.
Anayejitambua hujikita katika kutenda kuliko kusema tu.Huweka bidii katika kazi . Huanzisha na kutenda mambo ambayo hufaidisha viumbe wote . Husema pale inapohitajika,huheshimu mawazo yake na huwa tayari kuchukua malipo ya maneno yake mwenyewe.Hakimbii kivuli chake. Hayupo tayari kuona wengine wakikosa uhuru  kupitia yeye. Anatambua kuwa wakati wote huvuna alichopanda..

Anayejitambua huweka mkazo katika uhusiano mwema na nafsi zingine. Huthamini mahusiano yenye thamani. Mahusiano kwake hutokea ndani, hujengwa ndani na hivyo hudumu. Upendo kwake ni lugha ya moyoni, huleta furaha, mshikamano na amani.Zitokeapo changamoto katika mahusiano,huwa tayari kuyatatua kwa ajili ya kuyakuza zaidi.

Anayejitambua hutambua kuwa hapa duniani hatupo katika kushindana,ushindani kwake haupo,hushirikiana na ushindi kwake ni furaha katika kutimiza wajibu wake. Huandaa silaha zake ndani na kuteketeza kila kisicho na manufaa kwa binadamu. Baada ya milima na mabonde katika maisha yake ushindi huzaliwa ndani mwake. Hutumia uwezo wake kwa ajili ya Wengine na si dhidi ya wengine..

Huishi katika hali ya kujitolea na bidii. Huwa ni zawadi ya aina yake hapa duniani. Haogopi kutenda. Huendeleza mambo yaliyojenga utu,ubinadamu na misingi bora ya kuishi yaliyojengwa na binadamu waliomtangulia. Maisha yake hufundisha wengine.  Hutambua juhudi za wengine na wote wanaompa msukumo wa kutenda zaidi hasa pale anapokutana na  changamoto. Hutambua kuwa hayuko peke yake,bali dunia imejengwa kwa muungano wa nafsi zinazotimiza majukumu kwa dhati.

Haogopi ukweli hata pale unapoumiza. Hutoa nafasi ya kusamehe kila wakati anapokosewa. Hujisamehe yeye pia anapofanya makosa. Hushiriki katika ujenzi wa maisha yake.
Hutambua kuwa kila jambo hutoa fursa,kila kiumbe ana fursa. Hakusanyi ama kujilimbikizia kwa ajili ya sifa. Hutazama wengine kama anavyofanya kwa nafsi yake. Inapostahili hujitolea alichonacho,hutoa kwa wale walioshiriki kwa yeye kupata. Hutengeneza maisha yake yawe ya kutoa fursa kwa wengine badala ya kuwanyang’anya wengine .

Anayejitambua haichukuliai dunia kama chanzo cha maumivu bali hugundua kuwa dunia humpa kila mmoja kadiri anavyohitaji.Dunia husikiliza kutoka kwenye uwezo  ulio ndani mwetu tuliopewa na Mungu.Hata mara moja hajichukulii kuwa ni bora kuliko binadamu wengine na wala si dfhaifu kuliko wengine. Hutambua kushabihiana na kutegemeana kati ya kiumbe kimoja na kingine.Hivyo anatambua kuwa kama ikiharibu mazingira ,ni sawia na kuharibu nafsi yake.
Binadamu anayejitambua huyajenga na kuyatunza mazingira yanayomzunguka


Anayejitambua hamlaumu Mungu hata mara moja. Uhusiana wake na Mungu ni wa heshima,urafiki na huwa na umoja naye . Mienendo yake yote humwelekea Mungu .Anawaheshimu wanaoamini sawia naye na wasio amini sawia naye. Hashiriki kutumia imani ama dini kama njia ya  utengano kati ya binadamu,ama binadamu na mazingira yake.

Ni mfano wa sifa njema ya binadamu. Huchukua majukumu yake. Ana faida kwa viumbe wote.Hulinda, hujenga, huheshimu, Huishi vyema duniani. Ni mfano wa aliyeletwa kuifanya nuru ya Mungu ing’ae. Ni halisi,haishi maisha bandia. Ni wa kutumainiwa, si mbinafsi. Wakati wake kuwepo duniani ukifikia tamati,huondoka kwa furaha ya kutimiza alichotumwa,na kuacha dunia ikimlilia.Ni wewe na mimi.

Friday, August 30

Maisha yako yanaongea

 
matendo yako kwa wengine huonesha jinsi ulivyo

Ukitambua kuwa maisha yako ni ya thamani kwako na kwa wengine,unafungua ndani ya moyo wako kuishi kwa dhati.Sauti ndani mwako inaanza kusikika kwa viumbe wengine.Unapata thamani zaidi kupita vito vya thamani na zaidi ya fedha.
Maisha yako yanakuwa mwanga kwa viumbe wote.Unaanza kutumia kila kipawa na nafasi unayopewa na Muumba kwa ajili ya wote kwa utukufu wake yeye.Maisha yako yanaongea

Saturday, August 24

TAZAMA UPYA SABABU YA WEWE KUWEPO DUNIANI

Tangu tumboni kwa mama umepewa uwezo wa kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi.Umepewa vipawa mbalimbali ili kusudi la Muumba litimie…Unatambua kuwa licha ya changamoto nyingi unapaswa kufurahia uwepo wako duniani na kutolaumu dunia, viumbe na nyakati zake bali kupitia hivyo unayafanya maisha yako kuwa ni ya faida kwa dunia hii na viumbe vilivyopo…Kumbuka umezaliwa na upo duniani kwa sababu muhimu ya kipekee.hivyo ishi maisha yenye makusudi na matazamio
Unapaswa kukumbuka sasa kuwa upo duniani si kwa bahati tu bali kwa sababu maalum,kisha amsha moyo wako na nuru iliyo ndani mwako.Kumbuka kuwa sisi tu wamoja, kila mmoja akiwa na thamani sawa na mwenzake.Thamini kilicho ndani mwako kisha utatambua thamani ya wengine
Tupo kuangaza viumbe wote kwa kuwapenda,kuwajali,kuwathamini na kushirikiana  nao thamani ya ubinadamu.Walishe wenye njaa,wafariji yatima na wajane,visha wasio na mavazi..yote ni kuangaza nuru iliyo ndani mwetu hasa tunapofanya pasipo kutaka sifa wala malipo...Hupati kuwa na maisha ya thamani kama hutatenda kila jambo kwa msukumo wa moyo.

Wednesday, August 14

Nafsi huru

Kuna nyakati maishani mwetu ambapo vitu na watu walio karibu nasi watatutoka na kuwa mbali nasi, hii inatokea ili kutukumbusha kuwa tumetumwa kila mmoja kama nafsi huru yenye kazi maalum .Kila nafsi ni rafiki wa kweli wa nafsi yake . Inatukumbusha kuwa tusiishi maisha ya wengine bali kila nafsi ijenge maisha yake iliyoitiwa.Maisha na matukio yatutokeayo yanatukumbusha kutazama ndani mwetu palipo na nuru na sauti ya Muumba.Tunakumbushwa kurudi ndani yetu kila wakati tunaposukumwa na vitu vinavyotusahaulisha sababu ya kuwepo duniani.Yapo mengi yanayotugawa, kutupoteza na kutusahaulisha kuwa ss ni malaika tuliobeba miili kuiangaza nuru duniani kote.
Kila nafsi ipo sehemu muafaka kwa wakati na nafasi muafaka.
3Pia kila nafsi hutoka sehemu kwa wakati muafaka ili kuipa nafasi nafsi nyingine nafasi muafaka.
Nafsi isiyotumia nafasi ni nafsi isiyotambua sababu ya kuwepo-Katika ulimwengu halisi hakuna kufa,bali kubadilika kwa nafasi na kazi mpya.Nafsi itendayo jukumu lake huishi milele .Zikutanapo nafsi zitendazo wajibu huunda umoja uundwao kutoka ndani ya kila nafsi.Ni muungano takatifu ambapo dunia mpya huundwa na kisha matokeo yake kuonekana katika ulimwengu unaoonekana.Je wewe ni mmoja wa umoja huo?.Ishi maisha yako halisi.

Tuesday, August 6

Ugunduzi wa chemchem ndani yako

Safari kubwa ya ugunduzi ni juu ya maisha yako,ni safari ambayo utaamua kutafakari juu ya maisha yako-unatoka wapi na unakwenda wapi.Ni safari ambayo licha ya kuwa njia yake ni vipande vingi vya changamoto,utakuwa tayari kuvipitia na kuugundua uwezo ulionao“ukitambua.kuwa wewe ndiwe msanifu wa maisha yako na kila utendalo linaleta miujiza mipya duniani Mwishowe mafanikio yatakuja yakiwa ni mkusanyiko wa maamuzi na matendo yako.Picha yako uliyoijenga kwa fikra zako itakuwa halisi.Amini juu ya uwezo uliopewa na Muumba.

Saturday, January 5

ATHARI ZA MSUKUMO WA WANAOKUZUNGUKA

Watu wanaotuzunguka hutusukuma kufikiri na kutenda kadiri ya kanuni  na imani zao na kutufanya kuwa watumwa wa fikra za kimitazamo(picha na www.nlm.nih.gov)

Nilikwisha kujadili ni namna gani mafanikio ya mtu yanaanza ndani mwako,   soma zaidi hapa
Katika makala hiyo,tunajifunza kuwa kila jambo huanza na wewe.Chochote kinachoanza na msukumo utokao ndani yako,ndilo linaloleta mafanikio.Kwa kifupi tu mafanikio ya mtu yanaanza na yeye mwenywe na si msukumo utokao nje yake yeye.

Leo tutajadili jinsi msukumo wa nje (toka kwa marafiki,ndugu na wote wanaokuzunguka unavyowezakuathiri upekee wako na maamuzi.

Tumejifunzapia kuwa kila mmoja ni wa kipekee kwa maana ya nafsi yake na atasimami katika maamuzi yake na ujenzi wa maisha yake.Lakini tunaishi katika jamii ambayo inatutia msukumo wa kuamua na kutenda kadiri ya mawazo na kawaida yao.
Kabla hujazaliwa walikwepo waliotutanguli,kwa maana ya babu zetu na wengine wengi waliopita.Hawa walitengeneza mfumo yao ya maisha  ambayo tunaweza kuuita mfumo wa jamii,ambao ulijenga matarajio mengi ya watu mmojammoja  na jamii nzima.Mfumo huu ni pamoja na kanuni,mila ,desturi,imani,dini,serikali,sherehe.Mfumo huu umejengwa na sheria na kanuni nyingi ambazo unapozaliwa tu,unakuwa umefungwa moja kwa moja na mfumo huo pasipo kupenda ukiamini ndio mfumo sahihi.Sheria na kanuni zilizopo katika mfumo huu ulioukuta zinapokuwa kawaida kwako,zinaufanya mfumo wako wa tafakari uwe na uelekeo na fikra zilizo ndani ya mfumo huo.
Fikra zenye mipaka huleta matokeo yasiyo huru (picha kwa hisani ya www.rfidgeneral.com)


Mfumo huu unakulazimu kujifunza na kufuata mengi kama ni nini unapaswa kufuata,kuamini,ni nini kinakubalika na nini hakikubaliki,kipi ni chema na kipi ni kibaya.MFUMO HUU WOTE UNAKUPELEKA KUFUATILIA KILA JAMBO KADIRI YA TARATIBU NA MAWAZO YA MFUMO.Maka unapokuwa unakuwa na fikra za kimfumo kuwa jambo fulani lipo hivi tu,na hivyo mara nyingi hujenga mpaka wa kufikiri na kuamua.Unakuwa huwezi kufanya jambo mpaka usikilize waanaokuzunguka wanasemaje.
Natoa mfano wa mjomba wanguambaye pale alipotakakuoa binti ambaye walikubaliana na kupendana,alibadilisha uamuzio baada ya kuambiwa tu eti dini anayoiamini binti huyo si nzuri.Hapo dini ikawa juu ya upendo.
Pia kuna rafiki yangu mmoja alikuwa akijadili na marafiki juu ya imani ya dini nyingine,akashawishiwa kuifuata imani mpya,akakiri kuridhika na imani hiyo lakini hofu yake ikwa je,wazazi watanionaje?,licha ya kuwa yeye ni mkubwa kiumri.

Hii ni baadhi tu ya mifano.Mwisho kbisa tunaanza kuitazama  dunia kama sehemu ya ushindani.Tunajifunza uchoyo,ubinafsi,usiri na visasi kwa sababu ya mfumo licha ya kuwa yapo mengi mazuri.

Ushindani huo unatufanye tufikiri na kutenda kwa kuangalia mitazamo ya jamii.Unakuwa huna fikra za kutafakari jambo nje ya mipaka ya jamii.HIVYO unakuwa si huru katika maamuzi juu ya maisha yako mwenyewe.Kwa kifupi unakuwa mtumwa wa mfumo huu wa jamii.,ukifikiri na kutenda katika uwanja wa fikra za jamii.Ukweli ni kwamba usipotoka katika mpaka huu na kuuvuka,kuwa huru,hutaishi kamwe maisha yako halisi.
Maisha yetu ni matokeo ya fikrazetu (picha kwa hisani ya mtandao)


Ninachotaka kukisema hapa ni kuwa ukitaka kuishi maisha unayoyachagua wewe ,na kufikia mafanikio ni lazima uchukue uamuzi wa kufikiri nje ya mipaka ya mawazo ya jamii.Ni lazima uvunje mipaka ya mazoea na ile ya sheria na kanuni za imani ya jamii.Ni lazima ujifunze kuwa huru.Naomba nieleweke vizuri hapa si kwamba nahamasisha watu wavunje sheria za nchi ama mahalia,laaah,kuvunja mazoea ni kufikiri kwa mapana bila kufungwa na mawazo yanayoaminika tu na jamii.


Imani ya jamii ina nguvu sana,na hujenga upotofu ya kuwa tunapaswa kufikiri hivi na si vile,fulani yupo hivi na vile na inamsukuma mtu kutenda kadiri ya fikra za jamii husika.Tunalazimika kuishi maisha ya bandia ili tuonekane kwa wengine(Amini nakwambia utakuwa mtumwa katika mawazo mpaka pale utakapopanua wigo /uwanja wako wa fikra).

Unakuta jamii inaamini juu ya ushirikina na uchawi katika kutafuta mafanikio,hivyo kunakuwa na imani kuwa huwezi kufanikiwa mpaka uende kwa mganga.Watoto wakiugua magonjwa mabayo ni matokeo ya maisha anayoishi basdi inaaminika amechezewa(amelogwa).Tukumbuke kuwa mtu hawezi kukutendea ubaya  kama wewe si kisababishi cha fikra za mtu huyo kukufanyia ubaya.Nakumbuka kuna rafiki yangu ambaye nilisoma pamoja nae,alikuwa namsukumo sana kwa wengine,akiwaaminisha kuwa ili uwe bora na rafiki yake ni lazima uwe unakunywa pombe ama kuzisifia.Hii yote ni matokeo ya imani na fikra za kimfumo.

Hivyo tukumbuke kuwa kama tunaishi tukifikiri na kutenda kwa mipaka ya imani za wengine,basi sisi ni watumwa wa imani hizo mpaka pale tutakapotoka nje ya mipaka hiyo katika kufikiri na kutenda.Tunatafuta kukubaliwa na mawazo na mitazamo ya vikundi fulani.Tukumbuke kuwa picha halisi juu ya kinyago huwa sahihi kwa mchongaji,ambaye anachonga akiwa na picha yake katika fikra kuwa nataka awe hivi.Ukiwauliza wateja wanaonunua kinyago,kila mmoja atatafsiri kadiri ya fikra zake pia.
Mabadiliko katika fikra na maendeleo yako yanaanza pale unapoanza kufikiri nje ya mipaka ya wengine(picha kwa hisani ya mtandao)


Kwa nini uishi kwa mawazo ya wengine?Kwa nini uumie unapoambiwa una sura mbaya wakati hayo ni maoni ya msemaji tu.Ukitaka kupata majibu juu ya maisha yako,chimba ndani yako..Tafuta ndani yako.Ninaamini kila jambo huanza na wewe(mimi),Utajiri na mafanikio yote yanatoka ndani mwa muhusika.Zawadi kubwa juu ya maisha yako ni kuithamini nafsi yako  na kuisikiliza sauti kubwa itokayo moyoni mwako,ikuongozae juu ya kutenda,hii ni sauti ya Mungu iletayo mafanikio,furaha na kila lililo jema.Sauti hii inakupa nguvu ya kutenda miujiza kila wakati,ndiyo inayofanya nuru ya maisha yako ing'ae.

Jamii inakufanya ulazimike kuenenda kimawazo na fikra kadiri ya imani yake.Kwa nini usikuballi jinsi ulivyo na kuanza kuchimbandani yako palipo na siri kuu ya maisha yako?Mimi binafsi natambua jinsi ninavoonekana.Najikubali kwa kuwa mimi ni zaidi ya nilivyo.Ukiachilia mbali mazingira ninayoishi na sura yangu,mimi ni wa thamani,kama wengine.Wewe ni wa thamani jinsi ulivyo,na thamani yako ni sawa na binadamu wote.Unao uwezo wa kuwa na kuishi maisha ya furaha na mafanikio.Unastahili,wewe ni Matokeo ya kazi kubwa ya Mungu. 



Sasa anza kujikubali na kuepuka misukumo ya wale wanaokuzunguka.Anza kutazama uwezo ulio nao,tazama chemchem ya mafanikio iliyopo ndani mwako.Sisi sote ni bora .Sisi wote ni wamoja.
Huu ni wakati wa kujifunza kuwa wewe,kujikubali,kukua na kubadilika.Anzakujitambua wewe kisha utatambulika kwa wengine.Hongera kwa kujitambua

Ahsante. Joseph Pongu-0717903089,0765046644.Karibu tujadiliane na kuinuana.

HATUTAMUACHA HATA MMOJA 2013


Tumejifunza mambo mengi kwa mwaka 2012,ambayo yametufanya tutambue sisi ni akina nani na kwa nini tupo hapa duniani.Tumetambua kuwa sisi ndio wasanifu wa maisha yetu wenyewe.Tumejifunza kuwa kila jambo ni jema likitazamwa kwa mfumo chanya na kuwa mambo yote yatokeayo maishani mwetu ni matokeo ya fikra zetu na vitendo vyetu wenyewe...Tumejifunza kuwa upendo ndio silaha ya mafanikio ya kila jambo,upendo ni nuru.tumejifunza pia matokeo yake ambayo ni pamoja na furaha,amani,umoja,uvumilivu na ni mafanikio.Tukajifunza pia kuwa kinyume cha upendo ambayo ni chuki ndiyo matokeo ya maumivu,wivu,visasi,chuki,masengenyo na ndio matokeo ya kila jambo liletalo hasara katika maisha yetu
SISI NI WASANIFU WA MAISHA YETU WENYEWE
 

Leo hii tutajikumbusha kuhusu majukumu yetu …Mwaka mpya ulioanza tuuutazame kwa uchanya wake.Tuanze sasa kutimiza malengo yetu kila mmoja ya kuwepo hapa duniani.Kila mmoja wetu anayo majukumu yake.Kila mmoja ana wito unaomuita ndani mwake,ana sauti ya Mungu ndani yake inayomuita kutenda kwa ajili ya wengine na kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi

Hakuna hata mmoja wetu ambaye hatayapitia magumu,kwa sababu bila magumu kutokea hatuwezi kuendelea.Mwaka huu ni mwaka wa kusonga mbele ...tutasonga mbele,hatutamuacha hata mmoja nyuma
Ni mwaka ambao mwalimu anayeishi katika mazingira magumu yenye milima mingi,ataamka kila siku na kufundisha kwa bidii na kuwanyanyua wengine wengi.Anahitajika huyo ambaye hatalalamika na kusubiri serikali(kwani serikali ni kila mmoja wetu) bali atakuwa ni mfano wa kuigwa wa mbinu bora za kutatua matatizo.Mwalimu popote ulipo amka na kutenda kwa ajili ya wengine.Amka mwalimu.

Sauti ya upendo husikika kwa viumbe vyote.Huu ni mwaka wa kuwa nuru kwa wengine(picha toka helped by animals kwa msaada wa mtandao)


Ni mwaka ambao daktari ataamka mapema na kukumbuka jukumu lake ,ya kuwa hayupo tu kwa ajili ya kutazama idadi ya wagonjwa na kiasi cha fedha,bali yupo kwa ajili ya upendo,akijali utu wa wengine pasipo kubagua hali,kabila,rangi ama hali yeyote na daima atahesabu mafanikio yake kwa kuokoa wengine,kuwainua walio kata tamaa.....na hata akitokea mtoto akaulizwa upendo ni nini,basi amtazame daktari kwa ujasiri akisema......huu ndio upendo.

Ni mwaka ambao kila anayetoa huduma kwa wengine,atatoa akisukumwa na upendo.Kila atazamapo wengine,atambue kuwa anajitazama yeye,na kuwa thamani yake ni thamani ya wengine wote.Anapowatendea wengine akumbuke kuwa anaitendea nafsi yake.Ni mwaka ambao sisi tulio binadamu tutaonesha upendo uliotukuka,utakaofanya nuru ya Mungu iliyo ndani mwetu iwaangaze binadamu engine wasiotambua upendo,ili nao waishi maisha ya upendo.
Sisi ni wamoja,sisi wote ni wana wa Mungu,tofauti zetu zimejengwa na woga ,fikra zetu


Huu ni mwaka ambao tunapaswa kuifanya dunia kuwa sehemu bora,ili nasi tuwe malaika wa dunia hii.

Binafsi jiulize utamtendea nini yule Mungiu ambaye yupo ndani mwako?Je ukiwa katika nyakati za faragha na Muumba wako,utajivunia lipi ulilomtendea?Kumbuka kuwa kama huna malengo ya kutenda jambo lolote huwezi kutimiza lolote.Ni sawa na kusafiri safari isiyojulikana,mahali na hata uelekeo!Tukiweka malengo na kuamini katika kuyatekeleza,hakika yatatimia.

Mimi binafsi najisikia faraja sana kuhamasisha wengine na kuwasaidia wengine waweze kufikia mafanikio HASA PALE WANAPOKUWA NA MSUKUMO UTOKAO NDANI MWAO.Nimejitolea kwa ajiliya wengine na wakati wote najisikia faraja.Ninapokutana na magumu,ninayashinda kwa sababu naamini katika ushindi.Sisi  tumeumbwa kushinda.,na ushindi ni matokeo ya usanifu katika fikra za kila mmoja.

Ninapata faraja ninapoona kuwa yupo nesi ambaye licha ya kwamba anaumwa,anaamka na kwenda kazini kwa ajili ya wengine.Ninafarijika ninapoona kuwa yupo mtu ambaye licha ya kuwa na magumu mengi,anatenda ka ajili ya wengine pasipo kutegemea malipo.Nilikwenda kijijini nilipozaliwa,nikakutana na mama ambaye kipato chake ni kidogo,anaumwa kwa miaka mingi lakini anajitolea chakula na malazi kwa ajili ya wengine....anawafariji wengine,hata anapokuwa katika ugumu sana,hakati tamaa.Maisha yake ni nuru kwa wengi.Daima hamuachi jirani akiwa katika huzuni,nuru yake inaishi.Ni mwanga kwa waliokosa nuru.

Nafarijika kuona wengi ambao wanakwenda mbali na familia zao,mbali na wapendwa wao kwa ajili ya wengine. 
Nafarijika pia kuona wengi ambao wanajinyima kwa ajili ya wengine.Wengi wao wanaishi maisha ya kawaida,(kwa maana ya kipato) lakini wanatambua maana ya thamani yao kwa wengine,wapo tayari kujitolea pasipo kutambuliwa na wengine.Hii inanipa faraja ya kusonga mbele.Hwa wanatambua kuwa sisi binadamu wote ni wamoja ,tofauti zetu ni juu ya fikra zetu wenyewe.

Daima umoja ni nguvu.Usisubiri wengine wachukue hatua.Anza wewe.Mimi nimepata nafasi hii kwa kuandika.Wewe pekeyako pia watosha,unaweza kubadili wengine kwa kusamehe,kuimba,kufundisha,kutoa nakala nyingi za mafunzo kwa wengine,kwa kuwahurumia wengine,kutembelea wagonjwa,yatima,wafungwa na matendo yote yenye kuleta thamani kwa wanaotuzungua.Mwaka 2013 hatutamuacha mtu hata mmoja katika umasikini,chuki,uvivu,visasi,magonjwa huzuni...nk.Mwaka huu hatutamuacha yeyote kwenye giza.Tunao uwezo wa kuyatenda haya yote.Chukua hatua,mabadiliko yanaanza ndani yako.
Wathamini wengine,hata usiowafahamu....

Tujenge mwili mmoja,moyo mmoja na kupambana mpaka mwisho kwa ajili ya dunia iliyo bora na mafanikio kwa ajili yetu na wengine.

kila mmoja wetu anapochukua hatua licha ya vikwazo,tutayafika mafanikio(picha kwa msaada wa mtandao)




Tuishi maisha yetu kwa dhati bila uoga,tuchimbe ndani ya mioyo yetu ambapochemchem ya kila ushindi ipo,Tujifunze thamani yetu ,tuwathamini wengine kwa kuwa wao ni wa thamani kama tulivyo,tusamehe na kutazama mbele,tujali mawazo ya wenginena imani zao tuziheshimu.


Kila mmoja apende nafsi yake,ayapende maisha yake,asanifu vyema vyote vinavyomzunguka,KILA MMOJA AYAFANYE MAISHA YAKE YA THAMANI KWA WENGINE.Tutimize malengo yetu,yanayotokana na sauti iliyopo ndani mwetu,ili ule muda wa kuishi katika dunia hii unapokwisha ,na kifo kukuita,uitike kwa furaha,kwamba uliyaishi vyema,usipate hata sababu ya kuomba upewe tena muda,bali nuru ya maisha yako iwe mfano wa kuigwa milele.Uiage dunia na kuondoka kishujaa,kuelekea katika maisha mengine mapya yenye majukumu mapya.


Tutapita katika magumu mengi lakini daima tutasonga mbele,hatutamuacha yeyote nyuma,tutainuana sisi kwa sisi,hatutatazama nyuma,wala kuogopa kusonga kwa woga wetu,hatutaogopa lolote kwani sisi ni wa thamani,tutakumbuka daima kuwa dunia si sehemu ya ushindani bali ni sehemu ya ushirikiano na umoja na hivyo daima tutafikia tuendako,kwa sababu Mungu yu ndani mwetu.
Ahsanteni sana

Monday, December 31

UKWELI KUHUSU WEWE

Wewe ndiye mjenzi na mbomoaji wa maisha yako katika nyanja zote kwa fikra zako kwani fikra ndiyo mbegu ndani yako itoayo matokeo kadiri ya sababisho litokanalo na msukumo wa kimazingira. Hivyo mafanikio yako huja kwa kupanda fikra za mafanikio na kutofanikiwa huja kwa kupanda fikra za kushindwa,uma kwa kujua na kutojua.
Wewe ni msanifu na mjenzi wa maisha yako(picha na cognitivesocialweb.com)




Wewe ndiye unayebomoa na kuangamiza maisha yako kwa fikra zako,kwa kujua ama pasipo kutambua(picha na hot100tips.com)

Kamwe huwezi kufanikiwa kama hujui unachokitaka,huwezi kuona mbele pasipoonekana kama hufahamu uendapo,ni mpaka pale utakapojua unataka kuwa nani,ndipo utakapokuwa.....ni sawa na kwenda safari isiyojulikana hata uelekeo.

Mungu alipokuuumba alikupa nguvu na uwezo,akaifanya dunia na vyote vinavyokuzunguka vitii maagizo yako,hasa yale yanayotokana na msukumo wa moyo wako..hivyo wewe ni kiumbe bora jinsi ulivyoumbwa,wewe ni aidi ya ulivyo,wewe ni upendo,amani,faraja,chuki,visasi,wewe ni mwerevu,na msanifu wa maisha yako mwenyewe,hivyo hupaswi kumlaumu yeyote kuhusiana na jambo lolote linalohusu maisha yako,chukua hatua juu ya maisha yako mwenyewe.

Ndani yako ni chemchemi ya kila hali iletayo matokeo hasi ama chanya,ukifikiri kuhusu upendo utafute ndani yako,ukitaka kujua kuhusu uwezo ulio nao,utafute ndani yako,ukitaka kujua kuhusu mafanikio yako,tafuta ndani mwako...chemchemi yako haileti faida kama hujachukua maamuzi

Huna tofauti na binadamu mwingine kwa maana ya uwezo......anza kwanza kuuchunguza ubora wako uujue,ukiutambua,utambue kuwa wengine ni bora kama wewe,hivyo matendo yako yazingatie matokeo yake,fikra zako ziwe fikra njema juu yako na kwa wengine kwani kila utendalo kwa wengine,umejitendea mwenyewe.Maisha ni uchaguzi wako,na matokeo ya kila unachochagua ni juu yako.

Fikra zitokazo kwako ni sewa na bustani ama shamba,inaitaji kutazamwa na kupaliliwa...kuhakikisha kuwa unapanda mbegu bora,ukipanda mbegu isiyo bora (fikra mbaya dhidi yako na maisha yako) huleta matokeo sawia na mbegu uliyoipanda.

Maisha unayoyaishi hayatokei kwa kiitwacho bahati(nzuri ama mbaya) bali ni matokeo ya uchaguzi wako mwenyewe ama kwa kutambua na kutotambua.Umasikini,utajiri,furaha,huzuni,amani,chuki,upendo vyote ni matokeo ya uchaguzi wa maisha yako.Nguvu na uwezo wa kubadili matokeo hayo hutoka ndani mwako....Ni msukumo utokao ndani mwako pekee ndio utakaobadili maisha yako.

Kamwe wewe huvuti maishani vile vitu unavyovitamani ama maisha unayoyatamani,bali unavuta jinsi ya fikra zako.Fikra a ushindi huleta ushindi,fikra za kushindwa huleta kushindwa.

Mara nyingi unajaribu kubadili hali ama mazingira yanayokuzunguka pasipo kubadili fikra zako juu ya mambo hayo....Jinsi uvitazamavyo vitu huwa...ukilitazama jambo kwa uchanya wake,basi kila hali huwa ni nafasi,kama ni mtazamo hasi,basi matokeo yake huwa hasi na kwako huwa ni maumivu.

Friday, July 27

Tuachane Na Fikra Za Malalamiko, Upanuliwe Wigo Katika Ubunifu




Na: Meshack Maganga, Mjengwablog-Iringa.

Rais wa enzi hizo wa taifa la Marekani Theodore Roosevelt (Oktoba 27, 1858- Januari 6, 1919) alipata kusema, “What we need is more people who specialize in the impossible”, kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili ni kwamba, “Tunachohitaji ni watu wengi zaidi ambao wamebobea katika kufanya mambo yanayoonekana ama kudhaniwa kuwa hayawezekani, (specialists)”.

Kauli ya Roosevelt inanikumbusha habari ya vijana wawili waliohitimu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Vijana hawa walipokuwa chuoni muhula wa pili, mwaka wao wa kwanza wa masomo walibuni biashara ya usafiri wa bajaji. Walichanga shilingi laki nane kutoka fedha ya mkopo wanayopewa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu, ndipo wakanunua gari hiyo ya miguu mitatu na kufanya biashara hiyo ambayo iliwasaidia sana kuwakwamua kiuchumi.

Kwa mujibu wa maelezo yao ni kuwa wakati wakitambulisha wazo lao kwa wenzao waliambiwa “hilo haliwezekani!”. Wanasema kuwa katika kauli ambayo hawataisahau ni ile waliyoambiwa hivi, “Hiki kitabu cha UDSM kitawapaje muda wa kusimamia hiyo biashara yenu? Labda kama mpo tayari kwa supp zisizokwisha zitakazofuatiwa na disco”. Maneno hayo hayakuwazuia, walianzisha biashara wakaendeleza na bado walifaulu masomo yao. Wakafanikisha kisichowezekana!

Miaka ya karibuni watanzania tumeshuhudia kuanzishwa kwa utaratibu wa kuchangia gharama katika elimu ya juu. Suala hili ndilo lililopelekea kuundwa kwa bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Bodi hii hutoa mikopo kwa wanafunzi hao; katika viwango tofauti tofauti kutegemea na vigezo ambavyo imeweka kwa mujibu wa sheria na taratibu za uendeshaji wa bodi hiyo.

Mabadiliko ya mifumo ya gharama za elimu ya juu nchini Tanzania yanatupa somo muhimu sana kuhusu alama za nyakati. Ni suala la uhakika kuwa siku zijazo mchango wa moja kwa moja wa serikali katika kusomesha vijana wetu utafutika. Hapa naikumbuka kauli aliyopata kuisema Mkurugenzi wa shule ya Star International ya mjini Iringa, Madam Jessca, namnukuu, “Ninawekeza leo kwa kutoa sadaka na kuimarisha biashara zangu, ili siku Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itakapokosekana, wanangu wasishindwe kupata elimu ya juu” mwisho wa kunukuu. Hakuna haja ya kupambana na nyakati kwa kuzililia zama za Mwalimu J.K Nyerere ambapo elimu ilitolewa bure, bali tukabili nyakati zilizopo na kujipanga kwa nyakati zijazo

Tangu kuundwa kwa bodi hii kumekuwepo na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na mfumo huu wa uchangiaji wa gharama pamoja na utaratibu na utendaji wa bodi hii katika kufanikisha lengo hili.

Kuna wadau ambao kwa asilimia mia moja wanapingana na utaratibu huu wa kuchangia elimu ya juu na kuna kundi ambalo linaunga mkono. Sehemu kubwa ya kundi la pili inakwazwa na namna bodi hii inavyotenda kazi zake na kupelekea, mikopo kuchelewa kuwafikia wanafunzi kwa wakati husika, kukosekana kwa mbinu sahihi katika kubaini wapi wanastahili madaraja gani, pamoja na upendeleo (ama uzembe?) katika kupanga madaraja haya ya mikopo.

Bodi hii hutoa mikopo kwa madaraja kwa upande wa ada, “tuition fees” pamoja na fedha ya mafunzo kwa vitendo. Kuhusu fedha za chakula na malazi wanafunzi hupewa kiwango kinacholingana bila kuzingatia madaraja waliyopata. Hadi wakati huu bodi hii inatoa shilingi, elfu tano kwa siku, ama laki moja na nusu kwa mwezi, kama gharama za chakula na malazi.


Kumekuwa na changamoto zinazobainishwa na wanafunzi hawa kwamba kiwango cha fedha wanazopewa hazitoshi katika kuwawezesha kusoma kwa uzuri. Ingawaje vyuo hivi vipo katika maeneo tofauti tofauti, changamoto zinazowakabili wanafunzi hawa nyingi zinashabihiana.

Wanafunzi wengi wanatoka katika familia za kimasikini ambazo pengine hata 70,000/= ya kulipia ada katika sekondari walizotoka zilikuwa zinawapiga chenga. Sasa chukulia kuwa huyu mwanafunzi anapewa mkopo wa asilimia themanini, na yupo katika chuo ambacho gharama ya shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo ni 1,800,000/= Hii ina maana kuwa bodi ya mikopo itamlipia ada shilingi milioni moja na laki mbili na itampa shilingi milioni moja na laki mbili ya malazi na chakula kwa mwaka.

Katika ada atakuwa anadaiwa shilingi laki sita, (600,000/=). Hizi laki sita anatakiwa azilipe kutoka katika ile fedha ya malazi na chakula. Akilipa hizo ina maana anabakiwa na shilingi laki sita tu kwa mwaka wa masomo. (Isisahaulike kuwa bodi ina ukomo wa viwango vya kuwalipia ada wanafunzi inaowadhamini, ukomo huo ni milioni moja na nusu kwa mwaka wa masomo.) Laki sita kwa miezi nane ya masomo, kulipia pango, kununua chakula na kujipatia mahitaji mengine ya msingi kiuhalisia haitoshi.

Tatizo la mikopo isiyotosha elimu ya juu ni la kimtambuka kwa maana kuwa linahusisha pembe nyingi. Kuna suala la ada kubwa katika baadhi ya vyuo, kiwango kisichotosheleza cha fedha inayotolewa na Bodi ya mikopo kwa siku kwa chakula na mavazi, mfumo wa utoaji wa elimu ya juu nchini pamoja na fikra zilizopo miongoni mwa wanafunzi wengi wanaosoma elimu za juu.

Mwanazuoni mmoja wa nchi za Magharibi, G.K Chesterton amewahi kuelezea shida inayowakumba watu kupata ufumbuzi kwa matatizo yanayowakabili, yeye anasema “It isn’t that they cant see the solution. It is that they can’t see the problem” (Sio kwamba hawaoni ufumbuzi wa tatizo, ila ni kuwa hawalioni tatizo). Kuwa na tatizo ni kitu kimoja na kulielewa tatizo (chanzo cha tatizo, lilipo na madhara yake ikiwa halitatatuliwa) ni kitu cha pili. Tuna tatizo la mikopo isiyotosheleza kwa wanafunzi wa elimu ya juu lakini ufumbuzi wake umeendelea kuwa suala la kufikirika na imebaki kulaumiana.

Wanafunzi wa elimu ya juu na baadhi ya wadau wanadhani kuwa suluhisho la tatizo hili ni kuongezwa kwa kiwango cha mikopo. Serikali inasikia lakini haitendi kwa mujibu wa matakwa haya. Tayari pande mbili husika hazijakubaliana na ufumbuzi wa tatizo hili; ina maana kuwa eidha upande mmoja haujalielewa tatizo vizuri ama pande zote hazijalielewa.

Hata hivyo mwathirika mkubwa ni huyu mwanafunzi anayesomeshwa na bodi ya mikopo katika taasisi hizi.Hakuna namna zaidi ya mwanafunzi huyu kupanua wigo wa fikra zake na kuona ni namna gani ataishinda changamoto hii kwa mbinu na njia zilizo halali. Daima ufahamu uliopanuliwa katika njia mpya za kupata majibu ya changamoto, haurudi kamwe katika mipaka yake ya mwanzo. Zikomeshwe fikra za malalamiko, wigo upanuliwe katika ubunifu, badala ya mawazo ya kuilaani Bodi ya mikopo na serikali kwa mikopo isiyotosheleza ni vema kupanua fikra katika kujitegemea

Huu ni wakati ambao vijana wetu wanatakiwa kushusha chini vidole vyao vilivyoielekea serikali na kutazama ni nini kinaweza kufanyika kujikwamua. Mwanaharakati wa kweli hupambana kwa ajili yake na kwa ajili ya vizazi vyake vijavyo. Tujiulize, maswali yafuatayo. Je, vizazi vijavyo vitaishije pindi mchango wa serikali kwa elimu zao utakapofutika, ikiwa hatuweki misingi ya kujitegemea sasa? Vilio vyetu vimesikilizwa kwa kiasi gani? Je, tuendelee kulia ama tufute machozi, tujifunge mikanda tutazame tatizo kwa namna tofauti?

Hakuna maana ya kuweka nadhiri za chuki zitakazoliangamiza taifa kutokana na yale yanayopitiwa kwa sasa. Nafahamu wapo vijana wetu ambao kutokana na adha wanazozipata katika utaratibu huu wa mikopo, wananadhiri kuja kulipiza kisasi. Nao wanaweka nia za kuja kupukutisha rasilimali za taifa ili kunufaisha matumbo yao na ya ndugu zao. Vijana wetu wa vyuo vikuu lazima watambue jambo hili, ya kuwa uovu wa baadhi ya viongozi waliopo madarakani haupaswi kuhalalisha wengine kutenda maovu. Msomi ni lazima awe na ndoto za kuubadili ulimwengu wake kutoka hatua moja kwenda nyingine iliyobora zaidi.

Ipo haja kubwa sana kwa wanafunzi wa elimu ya juu kujijengea utamaduni wa kijasiriamali ili kwa fedha kidogo wanayokopeshwa waweze kuzalisha na kufidia upungufu unaojitokeza katika gharama za masomo yao. Nikigusia suala la ujasiriamali inawezekana kuwepo na vikwazo vingi, ikiwemo muda na mazingira ya kufanya huo ujasiriamali, ukosefu wa rasilimali (mitaji) na mengine mengi upendayo kuorodhesha. Anayevuka na kutatua vikwazo hivyo, huyo ndiye “specialist” wa yasiyowezekana!

Wanafunzi wengi waliopo katika taasisi zetu si wenye juhudi katika kufikiria, ubunifu na kufanya kazi kwa kujituma. Waangalie wanafunzi hawa jinsi wanavyoutumia muda wa likizo zao ndefu na fupi, mara nyingi hawafanyi kazi eidha za kulipwa ama za kujitolea. Mara nyingi hutoa sababu zinazosema na kuonesha kuwa hakuna kazi. Wananata, hawataki kukaa vijijini hata kama kuna fursa nyingi, wanataka kumalizia likizo zao Dar es Salaam.

Kuna wakati unaweza kudhani kuwa vyuo vya elimu ya juu hupendelea kufanya udahiri wa kimikoa, kwa sababu wengi wanataka kutambulika kama wakazi wa majiji hasa Dar es Salaam. Miezi mitatu ama mine ya likizo mtu yupo jijini kwa mjomba, binamu au kwa wa kutoka kijiji kimoja kule Songea, hana kazi zaidi ya kula, kulala, kuoga na kuangalia TV. Wakati mwingine analala sebuleni, na kulala kwake ni mpaka wote waende kulala! Kama mwanafunzi huyu angeenda hata kijijini kwenye kata ya nyumbani kwao akajitolea kufundisha shule ya kata kwa miezi minne angekuwa amezalisha angalau laki mbili!

Ninao mfano wa rafiki yangu mmoja ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Mzumbe, ambaye amekuwa mbunifu na alishaupiga teke ulimbukeni wa kujiona kuwa eti “wa elimu ya juu” kuna kazi hatakiwi kuzifanya hata kama zinamwingizia kipato. Huyu kila likizo huwa anarudi kijijini kwao na huko huutumia muda wote katika kufanya biashara ya alizeti. Huzunguka vijiji mbalimbali akikusanya na kisha kusafirisha alizeti hizo kwenda mjini. Katika moja ya likizo yake ya miezi minne, aliingiza mtaji wa shilingi laki tatu (fedha za bodi ya mikopo) na kuzalisha jumla ya shilingi milioni moja na laki sita.

Hawa wanafunzi wa vyuo vya juu, imewapasa kuwa na macho ya ndani yenye uwezo wa kuvumbua na kuzitumia fursa. Kuna kuwekeza kwa aina nyingi ambako wakati mwingine mtu si lazima awepo muda wote katika kusimamia alivyowekeza. Inawezekana kumiliki hisa katika makampuni, kuingia ushirika wa kibiashara (partnership) ama kuitumia jamii ya wanafunzi wanaowazunguka, kubuni biashara ama miradi itakayowaingizia vipato.

Pale juu katika makala haya nilitaja pembe zinazochangia mtambuka wa tatizo hili. Ingawa niliacha pembe zingine tatu, ni dhahiri kuwa zinachangia sana katika kufanikisha ufunguzi wa hizi fikra  za hawa wanafunzi wa elimu ya juu. Nitachambua pembe hizi katika makala mengine, lakini itoshe tu kusema, ukiwa na tatizo ni lazima ujikague na kujirekebisha vizuri kabla hujamvaa anaechangia kukua kwa tatizo lako.

Leo hata kama wanafunzi hawa wakaongezewa fedha na kulipwa 20000/= kwa siku, bado watagundua kuwa fedha hiyo haiwatoshi. Suluhisho sio kuililia serikali pekee wakati tumekaa na kubweteka. Tutalala, tutaamka, tutaandamana na kujikuta bado tuko pale pale. Badala ya kuwaza ukahaba, wizi na ujanja ujanja wa kukopeshana na kudhulumiana hebu wasomi wetu waanze kutumia taalveuma zao kufanya ubunifu na kujikwamua. Hii inawezekana ila kwa wale watakaojitolea ku-specialize katika yasiyowezekana.
 Na kila mwanafunzi wa elimu ya juu anayeguswa na hili analazimika kuwa specialist wa yasiyowezekana!

Thursday, July 12

DINI NA UUMBAJI WA WAAMINIO.

tazama Mungu umtafutae yupo ndani mwako
TAZAMA MUNGU UMTAFUTAE,YU NDANI MWAKO

Waimbaji huiwakilisha nuru ya Mungu kwa nyimbo.Waandishi pia hutufundisha yatokayo ndani mwao kwa kutumia maneno na kuyaandika.Wahubiri huifundisha nuru ya Mungu kupitia vipawa vya kuzungumza na kwa mifano mbalimbali hukumbusha uwezo wa Mungu ulio ndani mwetu.Mjasiriamali vivyohivyo hutenda kwa kutumia maneno yao ya kibiashara na bidhaa zenye kumjali mnunuzi.

Je wewe binafsi unaufundisha vipi utukufu wa Mungu?

Hakuna aliye hapa kwa bahati mbaya.Tuna sababu ya kuwepo duniani.
Nayo ni kufurahia uumbaji wa Mungu na kuitengeneza dunia bora.
Je,ni jinsi gani dini na imani ndani yake inatujenga kutambua sababu ya sisi kuwepo?

Nianze kwa kukusihi usome kuanzia mwanzo mpaka mwisho,ili uweze kuelewa ni nini nimekusudia kukifikisha kwako.....SI KAWAIDA KWANGU KUTAZAMA JAMBO KATIKA UPANDE HASI,lakini nitajadili upande hasi wa dini kwani ndicho kilichonisukuma kuandika kwa sasa,ninakusihi uchukulie hii kama elimu chanya ili ikusaidie kujadili na kujitambua.

 Dini inamaanisha jumla ya imani ya binadamu kadhaa pamoja na mafundisho wanayotoa kuhusu yale ambayo wanayazingatia ama kuyasadiki, yaani mambo ya roho, kama vile kuhusiana na Mungu, maisha na uumbaji-hii ndiyo maana ya kimtazamo kuhusu dini...Japo kimantiki hii si maana halisi.

Kila anayeingia katika imani hii,ama dini,matazamio yake huwa ni kwamba,dini itakuwa ni suluhisho la kila jambo kwa binadamu.....dini inatazamiwa kuwa ndio amani,ndiyo furaha,ndio umoja,ndio huruma,ndio usawa,ndio kila chimbuko la ubinadamu,na kikubwa kumfanya binadamu ajitambue yeye ni nani,anatoka wapi na anakwenda wapi......

Lakini kwa sasa imekuwa ikiwafanya binadamu kuwa tegemezi,wasio huru katika kila nyanja ikiwemo uhuru wa kufikiri usio na mipaka,uhuru wa kuchagua(simaanishi uchaguzi mbaya). Dini imekuwa kifungo cha kuwafanya wengi wasitumie vipawa walivyonavyo na hata wasisikilize sauti ya Mungu inayowatuma kutenda kwa ajili ya utukufu wake.(Unaweza kuuliza kivipi,jibu ni fupi...imani nyingi katika dini zimeweka mipaka ,inayomfanya muamini asifikiri juu ya hapo)NA KUWAFANYA wawe na maisha yasiyo na mwelekeo wa ushindi na hivyo kuamini kinyume na matarajio ya imani yenyewe.

1.KUMWOGOPA MUNGU
  Dini nyingi zimewafanya waumini wake wamwogope sana Mungu na kumuona kuwa ni adui.Wengi wamekuwa wakimuona Mungu ya kuwa yu mbali sana nao,asiye rahisi kufikika,asiye rahisi kuongea nae.

Wanasahau ya kuwa Mungu wamtafutao na kumwogopa yupo ndani mwao..Nae ni sauti iliyo kubwa kuliko utashi wa mtu mwenyewe,kuliko awazaye mtu,.Wanasahaulika ya kuwa yeye huzungumza na yeyote yule ,kwa wakati wowote pale kila mmoja awaye tayari kumsikiliza.

NAYE NI RAFIKI MKUBWA WA NAFSI YA KILA MMOJA WETU, Mungu ni mpole,mwenye huruma,asiyetazama tutazamavyo sisi,bali hutazama mawazo ya mioyo yetu,naye hujibu maombi ya mioyo yetu,na si maneno yatokayo kwa mtu..

 Hivyo kwa matokeo hayo dini hujenga jamii ya watu wenye kujiogopa wenyewe,wakimwogopa Mungu aliye rafiki mkuu,wakiishi maisha bandia ya kujionesha kwa wengine hasa wale wanaowaongoza,wawaone ya kuwa wamejaa nguvu za Mungu na matendo yaliyotukuka,huku wakifanya kinyume kwa siri(siri kwa binadamu wenzao,lakini Mungu ambaye tupo nae nafsini mwetu anatutazama kwa ubandia wetu)

2.KUISHI MAISHA YA WENGINE 
Dini zimekuwa zikiwafundisha na kuwafanya watu waishi maisha ya wengine na kuchagua maisha ya wengine waliopita na kuyaacha yetu yale tuliyoitiwa ili nuru yetu ing'ae kwa wengine....Hapa naomba nieleweke vizuri kuwa viongozi wengi wa dini wamekuwa wakiwafundisha watu kuishi kama fulani aliyepita(wapo wanaowaita watakatifu,wengine viongozi wao waliopita....)wakijitesa,wakijinyima pasipo sababu ya msingi,(SABABU ISIYO MSUKUMO WA MHUSIKA BALI MSUKUMO WA NJE}na matokeo yake kuishi maisha yasiyo ya furaha kwani mwisho hugundua ya kuwa furaha huja pale unapoishi maisha uliyoitiwa wewe mwenyewe,
Ukiyaishi kwa kujitolea si kwa ajili ya kuneemeka,bali ili wengine waitambue nuru ya Mungu aliyo ndani ya kila mmoja,na wale wasioamini ,wajitambue na kuiishi.

Dini zitakufundisha kuishi maisha ya wengine na matokeo ya wengine lakini ROHO WA MUNGU aliye ndani mwetu hutufundisha kuishi maisha yetu halisi ili tufikie katika matokeo mapya,yamtangazaye Mungu na utukufu wake.
Wengi wameingia kwenye mkumbo kwa kufuata tu imani ,kwa sababu ni za wazazi wao

3.DINI NA WATEULE

Dini hutoa picha ya matabaka,ya walio wakuu kuliko wengine,na wale wanyonge(watawaliwa) wanaosubiri pia kupewa ukuu na Mungu.inatokeaje? Viongozi wengi wa dini wamekuwa wakijipa ukuu na kuwaaminisha wengine kuwa ukuu huo umetoka kwa Mungu.Viongozi hawa wamejitangazia utawala,wakichuma kutoka kwa wengine ambao daima huwaogopa na kuhisi labda,Mungu kateua baadhi,na kwamba wao si wateule.

UKWELI NI KWAMBA,KILA MMOJA YU SAWIA KWA 
MUNGU,Yu bora akiwa na uwezo na nguvu za kuponya,kuamsha upya ari ya kila kitu,kulea,kuwanyanyua wanyonge badala ya kuwakandamiza,na ukweli ni kwamba,kwa sababu tuu mfano wa Mungu(tukifanana katika nguvu )tunauwezo wa kufanya chochote kile,kuyafikia mafanikio makubwa,kuvumbua vitu vipya,mradi tu tumetambua uwezo huu na kuchagua kuutumia  

aliye mkuu yu ndani mwetu,sote tu bora
kila mmoja akitumia kipawa chake vyema,basi huwa mkuu..tukumbuke aliye mkuu ni yule atendaye yote kwa ajili ya wengine pasipo kutegemea malipo,aliye tayari kuona wengine wakinyanyuka na kuendelea mbele,asiyetengeneza matabaka,ambaye kwake kila mmoja ni sawa,na katika yote,upendo humsukuma kutenda

Tunaweza kuyaona matokeo ya dini,ni jinsi gani inaumba mustakabali wa waamini wake dini zimekuwa ni chanzo kikuu cha matabaka na ubaguzi duniani hasa kutoka kwenye imani na mafundisho ya msingi ya imani husika,dini moja hujiona ni bora kuliko nyingine...tena zinawafanya baadhi kujiona wao ni wateule na kutengeneza tabaka la wanyonge tofautti kabisa na makusudio ya MUngu.mf. mkatoliki anajiona ni bora na ni mteule ukijilinganisha ma mlutheri,mkristo anajitazama kama ni mteule akijilinganisha na mwislamu.mlokole anajipa sifa ya kuwa mteule pekee wa mungu akijilinganisha na wengine...hili ni kinyume kabisa na malengo ya Muumba ya kumuumba kila binadamu na kumfanya kuwa sawa na mwingine..dini zimeleta imani iliyopelekea matabaka..choyo,majivuno,utengano na hata kutowasaidia wengine kwa kuwaona si wa darajasawia... tukirejea vita na vurugu nyingi ni zile ziletwazo na dini...rejea ireland,nigeria,sudan,uturuki zamani.....tena hizi ni vita kati ya dini kubwa zinazofundisha usawa na upendo lkn zikishindwa kuonesha matokeo bora... dini pia zimekuwa ni chanzo cha kumfanya binadamu kuwa mtumwa wa mawazo yake naa mazingira yake...zinafundisha kinyume cha makusudio ya MUumba ya kumfanya binadamu kuwa huru na kuyatawala mazingira yake...zinafundisha utegemezi huku viongozi wakuu wakiwatumia waumini wao kama daraja la kujipatia utajiri na utawala...

Mbele za Mungu hakuna aliye mkuu na wala mtawala...kila mmoja amepewa nguvu na uwezo na anapaswa kuzitumia kama nuru ya utukufu wake MUNGU hapa duniani... Ni WAKATI SASA KUTAMBUA YA KUWA DINI ya kweli ya kila mmoja,ipo ndani mwake...na kuwa ukitambua hilo,utakuwa huru,mawazo huru yasiyo na mipaka,kila jambo litawezekana na li ndani ya uwezo wako kwani Mungu aliye suluhisho la yoote,yu ndani mwako.

Lengo langu si kupinga uwepo wa dini,lengo langu ni kukufanya ujitambue na unyanyuke,uwe na hofu ya kweli,hofu ya kuona unamaliza uwepo wako hapa duniani pasipo kuifanya nuru ya Mungu iliyo ndani mako,ing'ae......hofu ambayo itakufanya utumie maisha yako yote kuwainua wengine.....walio wahitaji,walio wanyonge,walio wafungwa na kila mmoja ambaye upendo tu,huwaamsha

Friday, July 6

YOU ARE ALREADY PERFECT

are already perfect — you just need to realize it. You don’t need anything to solve this problem — you already have it. You just need to practice, like it’s the most important thing in your life, because in many ways, it is. ‘You yourself, as much as anybody in the entire universe, deserve your love and affection.’ ~Buddha

Tuesday, July 3

ISHI MAISHA YAKO HALISI

Kwa nini unasikitika kuwa vile ulivyo,kwa nini unatamani kuwa na mwonekano kama WA MTU FULANI...kwa nini unatamani kuiga fulani ili uwe maarufu ama ufanane nae?hii ni dalili ya kutotambua wewe ni nani..... wewe ni wa pekee,hakuna aliye kama wewe,hakuna mwenye kipawa kama ulichonacho,hakuna mwenye mfano wako....wewe ni wa kipekee toka kuumbwa kwako.....ni zaidi ya sura unayoitazama na kulaani ni kwa nini upo vile ulivyo.....tambua kuwa ndani mwako wewe ni zaidi ya hivyo ulivyo...ndani yako kuna uwezo mkubwa sana wa kutimiza kila jambo unalolihitaji...... vivyo hivyo ndivyo mungu kakuumba ukiwa wa kipekee...kakupa uwezo wa kila jambo ulitakalo...kakupa na uhuru wa kuchagua jtambue sasa na uyaishi misha uliyokusudia....amua leo ya kuwa utajikubali ulivyo na kusimama wewe ,kuishi maisha yako yaliyo halisi,kwa upendo huku ukitimia yote kwa nguvu zako zote,moyo wako wote ....hakikisha unasimama katika dira uliyojiwekea..pambana hata mwisho..na hakika utapata furaha ya kweli..katika maisha hakuna vita kubwa utakayokutana nayo kama ile utakayopigana kuwa wewe na kuishi maisha yako,kwani kila wanaokuzunguka wanataka uchague maisha wanayoyataka wao....tambua ya kuwa wao wanao pia uhuru wa kuchagua....wana uhuru wa kuishi maisha yao........ kuwa wewe,kuwa halisi,kuwa mdadisi na mvumbuzi ,kuwa wa pekee ilio pale utakapo maliza safari yako hapa duniani,dunia ikulilie nao wakaao ndani yake wakulilie,si kwa sababu ya kufa kwako,bali kwa alama yako iliyotukuka,iliyojaa upendo na thamani kwa bina damu wote....iliyojaa somo ya kuwa...hakuna kisichowezekan kwa binadamu na kwamba mafanikio huja tu pale mtu anapoamua kutembea ktk njia yake ambayo wengine walisema haiwezekani KUWA HALISI..ISHI MAISHA YAKO HALISI