Siku moja,pasipo kujua mkulima aliokota yai la tai.Kwa kuwa
hakutambua kuwa ni la tai,alilichukua na kupeleka kwa kuku ambaye alikuwa
ameanza kuatamia akalichanganya na mengine ambayo tayari yalishaanza kuatamiwa.Kuku
naye hakuweza kutambua utofauti wa yai hilo na mengine,akaliatamia.
Bada ya kuatamiwa kwa muda wa kutosha ,yai la tai
likatotolewa tai kati ya kuku .Tai huyo wakati akikua,alibeba tabia za kuku,ya
kukwaruza,kucharura na kudonoadonoa Akawa akiruka umbali mfupi tu sawa na kuku , akila
nafaka na wadudu,na hata akawa akiamini kabisa kuwa yeye ni kuku na sio tai.
Siku moja tai huyo akataza juu akaona kiumbe akiruka juu
sana angani na kuzunguka juu sana.Akashangaa na kuuliza ni kiumbe gani anayeweza
kuruka juu kiasi kile na kuzunguka kwa mwendo kasi namna ile.Akamuuliza kuku
aliyekuwa jirani yake,yule ni kiumbe gani anayeweza kuruka juu kiasi kile?Kuku
akamjibu."Ni tai.,ndege mwenye uwezo kuliko ndege wote.Tai akasema,Nataka
kuwa kama ndege huyo.”
Kuku akacheka kwa mshangao,Huwezi kuwa tai",wewe ni kuku.Tai
akaendelea kudonoa wadudu na kusema,"Ni kweli,mimi kuku sitaweza kuwa tai
,upo sahihi." na kuridhika na maelezo ya kuku ambaye aliamini kuwa hawezi kuwa bora kama tai.
Kwa miaka yote tai huyo akiendelea kuishi maisha sawia
na ya kuku akiamini yeye ni kuku,asijue ya kuwa yeye ana uwezo mkubwa ndani
mwake.Hakujaribu wala kuthubutu hata mara moja kula chakula cha aina tofauti na
kile anachoona kuku wenzake wakila.Aliaminishwa kuwa jambo jingine lolote zaidi
ya wafanyalo kuku,haliwezekani.Alipokufa alikufa akiwa ni kuku.
Kabla hujazaliwa walikwepo waliotutanguli,kwa maana ya babu zetu na wengine wengi waliopita.Hawa walitengeneza mfumo yao ya maisha ambayo tunaweza kuuita mfumo wa jamii,ambao ulijenga matarajio mengi ya watu mmojammoja na jamii nzima.Mfumo huu ni pamoja na kanuni,mila ,desturi,imani,dini,serikali,sherehe.Mfumo huu umejengwa na sheria na kanuni nyingi ambazo unapozaliwa tu,unakuwa umefungwa moja kwa moja na mfumo huo pasipo kupenda ukiamini ndio mfumo sahihi.Sheria na kanuni zilizopo katika mfumo huu ulioukuta zinapokuwa kawaida kwako,zinaufanya mfumo wako wa tafakari uwe na uelekeo na fikra zilizo ndani ya mfumo huo.
Fikra zenye mipaka huleta matokeo yasiyo huru (picha kwa hisani ya www.rfidgeneral.com) |
Mfumo huu unakulazimu kujifunza na kufuata mengi kama ni nini unapaswa kufuata,kuamini,ni nini kinakubalika na nini hakikubaliki,kipi ni chema na kipi ni kibaya.MFUMO HUU WOTE UNAKUPELEKA KUFUATILIA KILA JAMBO KADIRI YA TARATIBU NA MAWAZO YA MFUMO. Unapokuwa unakuwa na fikra za kimfumo kuwa jambo fulani lipo hivi tu,na hivyo mara nyingi hujenga mpaka wa kufikiri na kuamua.Unakuwa huwezi kufanya jambo mpaka usikilize waanaokuzunguka wanasemaje.Tai aliamini kila jambo aliloambiwa na tai kwa sababu tu ni desturi.
Mwisho kabisa tunaanza kuitazama dunia kama sehemu ya ushindani.Tunajifunza uchoyo,ubinafsi,usiri na visasi kwa sababu ya mfumo licha ya kuwa yapo mengi mazuri.
Ushindani huo unatufanye tufikiri na kutenda kwa kuangalia mitazamo ya jamii.Unakuwa huna fikra za kutafakari jambo nje ya mipaka ya jamii.HIVYO unakuwa si huru katika maamuzi juu ya maisha yako mwenyewe.Kwa kifupi unakuwa mtumwa wa mfumo huu wa jamii.,ukifikiri na kutenda katika uwanja wa fikra za jamii.Ukweli ni kwamba usipotoka katika mpaka huu na kuuvuka,kuwa huru,hutaishi kamwe maisha yako halisi.
Maisha yetu ni matokeo ya fikrazetu (picha kwa hisani ya mtandao) |
Ninachotaka kukisema hapa ni kuwa ukitaka kuishi maisha unayoyachagua wewe ,na kufikia mafanikio ni lazima uchukue uamuzi wa kufikiri nje ya mipaka ya mawazo ya jamii.Ni lazima uvunje mipaka ya mazoea na ile ya sheria na kanuni za imani ya jamii.Ni lazima ujifunze kuwa huru.Naomba nieleweke vizuri hapa si kwamba nahamasisha watu wavunje sheria za nchi ama mahalia,laaah,kuvunja mazoea ni kufikiri kwa mapana bila kufungwa na mawazo yanayoaminika tu na jamii.
Imani ya jamii ina nguvu sana,na hujenga upotofu ya kuwa tunapaswa kufikiri hivi na si vile,fulani yupo hivi na vile na inamsukuma mtu kutenda kadiri ya fikra za jamii husika.Tunalazimika kuishi maisha ya bandia ili tuonekane kwa wengine(Amini nakwambia utakuwa mtumwa katika mawazo mpaka pale utakapopanua wigo /uwanja wako wa fikra).
Unakuta jamii inaamini juu ya ushirikina na uchawi katika kutafuta mafanikio,hivyo kunakuwa na imani kuwa huwezi kufanikiwa mpaka uende kwa mganga.Watoto wakiugua magonjwa mabayo ni matokeo ya maisha anayoishi basdi inaaminika amechezewa(amelogwa).Tukumbuke kuwa mtu hawezi kukutendea ubaya kama wewe si kisababishi cha fikra za mtu huyo kukufanyia ubaya.Nakumbuka kuna rafiki yangu ambaye nilisoma pamoja nae,alikuwa namsukumo sana kwa wengine,akiwaaminisha kuwa ili uwe bora na rafiki yake ni lazima uwe unakunywa pombe ama kuzisifia.Hii yote ni matokeo ya imani na fikra za kimfumo.
Hivyo tukumbuke kuwa kama tunaishi tukifikiri na kutenda kwa mipaka ya imani za wengine,basi sisi ni watumwa wa imani hizo mpaka pale tutakapotoka nje ya mipaka hiyo katika kufikiri na kutenda.Tunatafuta kukubaliwa na mawazo na mitazamo ya vikundi fulani.Tukumbuke kuwa picha halisi juu ya kinyago huwa sahihi kwa mchongaji,ambaye anachonga akiwa na picha yake katika fikra kuwa nataka awe hivi.Ukiwauliza wateja wanaonunua kinyago,kila mmoja atatafsiri kadiri ya fikra zake pia.
Mabadiliko katika fikra na maendeleo yako yanaanza pale unapoanza kufikiri nje ya mipaka ya wengine(picha kwa hisani ya mtandao) |
Kwa nini uishi kwa mawazo ya wengine?Kwa nini uumie unapoambiwa una sura mbaya wakati hayo ni maoni ya msemaji tu.Ukitaka kupata majibu juu ya maisha yako,chimba ndani yako..Tafuta ndani yako.Ninaamini kila jambo huanza na wewe(mimi),Utajiri na mafanikio yote yanatoka ndani mwa muhusika.Zawadi kubwa juu ya maisha yako ni kuithamini nafsi yako na kuisikiliza sauti kubwa itokayo moyoni mwako,ikuongozae juu ya kutenda,hii ni sauti ya Mungu iletayo mafanikio,furaha na kila lililo jema.Sauti hii inakupa nguvu ya kutenda miujiza kila wakati,ndiyo inayofanya nuru ya maisha yako ing'ae.
Jamii inakufanya ulazimike kuenenda kimawazo na fikra kadiri ya imani yake.Kwa nini usikuballi jinsi ulivyo na kuanza kuchimbandani yako palipo na siri kuu ya maisha yako?Mimi binafsi natambua jinsi ninavoonekana.Najikubali kwa kuwa mimi ni zaidi ya nilivyo.Ukiachilia mbali mazingira ninayoishi na sura yangu,mimi ni wa thamani,kama wengine.Wewe ni wa thamani jinsi ulivyo,na thamani yako ni sawa na binadamu wote.Unao uwezo wa kuwa na kuishi maisha ya furaha na mafanikio.Unastahili,wewe ni Matokeo ya kazi kubwa ya Mungu.
Sasa anza kujikubali na kuepuka misukumo ya wale wanaokuzunguka.Anza kutazama uwezo ulio nao,tazama chemchem ya mafanikio iliyopo ndani mwako.Sisi sote ni bora .Sisi wote ni wamoja.
Huu ni wakati wa kujifunza kuwa wewe,kujikubali,kukua na kubadilika.Anzakujitambua wewe kisha utatambulika kwa wengine.
Vumbua uwezo ulionao.Tumia uwezo ulionao kupaa juu ya
mipaka unayofikiri ipo.Fanya yale unayoyakusudia maishani na uwe vile
unavyotaraji kuwa.Umezaliwa kuwa kiongozi wa maisha yako na kuyatawala
mazingira yako.Unaweza kupaa juu zaidi na zaidi pasipo kudondoka.Mipaka ulionayo
ni ya kifikra tu.Usiruhusu fikra za wanaokuzunguka zikufanye uwe na mawazo
mgando ama yenye mipaka.Huwezi kuruka juu kama utabaki na fikra kama za kuku na
kuendelea kukwaruza na kudonoa tu.Amua sasa kuruka.
Karibu tujadiliane
Pongu Joseph F-0717903089,0765046644