fikra za kila mtu hazijifichi,matokeo yake huleta tabia,tabia huleta matokeo hasi ama chanya(picha ya Hayati baba wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere) |
Fikra ni sawa na mbegu ndani ya maisha yetu..Unapopanda
mbegu kwenye udongo,matokeo yake huota kile ulichokipanda,kama
umepanda mahindi,utavuna mahindi.Vivyohivyo ,jinsi unavyofikiri(unavyowaza),unapanda mbegu
katika mitazamo na mienendo ya maisha
yako na matokeo yake huonekana sawia na fikra zako.
Ni wazi kuwa huwezi kupanda
mahindi ukavuna machungwa,vivyo hivyo huwezi kupanda mbegu itokanayo na fikra
za kushindwa,umasikini,huzuni,kisha ukapata matokeo ya maisha mazuri,furaha na amani.Hivyo ni wazi
kuwa ukitaka jambo jema litokee,anza kupanda kwanza fikra za wema(jambo hilo).Ukitaka
kupata matokeo mazuri katika mahusiano anza kwanza kupanda mbegu ya mtazamo
chanya juu ya mahusiano,upendo na furaha.Kama matarajio yako ni kuona dunia yenye
mazingira mazuri na bora kwa viumbe wote,anza kwanza kupanda fikra ya wema na
kujali viumbe wengine.Ukitaraji kuona mwenzi wako ana mwenendo mwema,anza
kupanda mbegu ya ushirikiano,upendo,kujali badala ya kufikiri kuwa kuna jambo
nje yako wewe,ama nguvu nje yako itakayoleta mabadiliko maishani mwako.Fikiri
vema juu yako ubadili maisha yako.
Muonekao wa mazingira yanayotuzunguka ni matokeo ya fikra zetu wenyewe |
Mawazo uwazayo juu yako ni kipimo unachojipimia katika
mwenendo na matokeo ya maisha yako.Matokeo yake kamwe hayajifichi.Hatuchagui
mojakwa moja juu ya mtiririko wa maisha yetu,lakini kupitia fikra,tunachagua
matokeo ya maisha yetu na kuujenga mtiririko wa maisha yetu.
Mazingira huchangia sana binadamu kuwa na fikra Fulani juu(dhidi)
yake.Mfano,mtu aishiye katika mazingira ambayo ni ya kipato cha juu,fikra zake
huwa mara nyingi si za kushindwa jambo tofauti na aliye katika mazingira yenye
vikwazo vingi.Anayepita kwenye magumu mengi,anapojitambua huweza kufanya mambo
makubwa kuliko aliyeko kwenye mazingira yasiyo na vikwazo vingi kwa sababu huanza kuwa na fikra za ushindi.
Tunapofikiri hasi juu ya maisha yetu,tunapata matokeo
hayohayo.Tunapofikiri chanya na kuchukulia kila jambo ama mazingira kama
nafasi,matokeo yake ni kukua zaidi na kusonga mbele.Tunachokipata maishani ni
matokeo yenye uasilia ndani mwetu na si nje yetu.Tabia za marafiki ulionao ni
picha ya tabia ulionayo wewe.Matokeo ya mafanikio ama kutofanikiwa kwa wewe na
unaowaongoza ni picha ya fikra ulizonazo pamoja na unaowaongoza.
Ukijitazama kwenye kioo,unaiona sura yako.Kama una
makovu,si tatizo la kioo,ni uhalisia wa jinsi ulivyo.Tabia unazoonesha nje,ni
picha halisi ya fikra zako ndani mwako.
Unaweza kujifunza fikra,tabia na mienendo ya jamii kwa
kuangalia matokeo yake.Jamii yenye umasikini,maradhi na ujinga ni picha halisi
ya fikra zao,elimu yao na mitazamo yao.Ukiona katika jamii wapo watu wanaopenda
kutembea wakiwa nusu uchi,ni picha kamili kuwa wengi wa wana jamii hiyo
wanapenda tabia hiyo.Mbuzi hawezi kuzaa kondoo,na kinyume chake ni sawia.
Wapo wanaodhani kuwa fikra alizonazo mtu huweza kuwa
siri.Ukweli ni kwamba matokeo ya matendo yako,ni matokeo ya mawazo yako.Fikra
zetu huonesha matokeo sawasawa na msukumo wake.Anayefikiri dunia ni sehemu
mbaya,huishi akiishutumu dunia siku zote.,Anayefikiri watu wanaomzunguka ni
kikwazo kwake,huishi daima ikawaona kuwa ndio sababu ya matatizo yake.Fikra
huonekana matokeo yake haraka kwenye tabia,na tabia huleta matokeo ya maumivu
ama furaha (majuto ama furaha).Kwa kifupi tabia uliyonayo,iletayo matokeo yake
ya majuto ama furaha ndiyo inayotoa picha ya fikra iliyotoa msukumo wa matokeo hayo..
Fikra yenye woga,wasiwasi,na kutowajibika huonesha tabia ya
unyonge , kutojiamini na kutochukua hatua,matokeoa yake ni kukata tamaa, kushindwa
na kuwa tegemezi kwa kila jambo.
Nazo fikra yenye
uvivu hupelekea tabia za udhaifu/unyonge, udanganyifu(usanii sanii) na matokeo
yake ni kuwa ombaomba,masikini na uzembe.(ukiona nchi ina kila rasilimali,na
inakuwa masikini,basi ujue watu wake wote ni wavivu kufikiri na wasipobadili
fikra hizo watabaki kuwa ombaomba hata kama matrilioni ya pesa yatatolewa kama
msaada)
Fikra za chuki na kutojiamini huleta tabia za visasi na
uonevu,matokeo yake ni vurugu,kutoweka kwa amani,mauaji ya kutumia nguvu.Unaweza
kujifunza matokeo ya viongozi wasiojiamini na wenye chuki.
Fikra za ubinafsi (umimi) huleta tabia ya ushindani,unyang’anyi,(roho
mbaya tunaita waswahili).Na matokeo yake kila mmoja anayajua.
Kwa upande mwingine fikra zote njema huleta matokeo mema kwa watu wote.
Fikra za kutia moyo,kujiamini na kuchukua hatua huonekana
katika tabia za utu wema na kuwajibika,matokeo yake ni amani,mafanikio na uhuru
wa kweli.
Huwezi kuwa huru mpaka utakapokuwa na fikra huru.Ukifahamu jinsi
unavyoweza kubadili maisha yako kwa kubadili fikra zako…umeyafikia mafanikio…usikate
tamaa.