Nuru Ndani Yako

Nuru Ndani Yako
Nuru Ndani Yako
Subscribe For Free Updates!

We'll not spam mate! We promise.

KARIBU SANA

HONGERA KWA KUCHAGUA BLOG HII.MAISHA NI UCHAGUZI...NA KILA UCHAGUZI NI SAHIHI....KILA UCHAGUZI UNA MATOKEO YAKE.......KUCHAGUA KUSOMA YALIYO KATIKA BLOG HII KUTAKUFANYA UJITAMBUE,,UUJUE UWEZO MKUBWA ULIO NDANI MWAKO NA HIVYO KUFIKIA MAFANIKIO UNAYOYAKUSUDIA........WEWE NI ZAIDI YA UJIONAVYO,NI ZAIDI YA UJIPIMIAVYO.....UTATAMBUA YA KUWA MUNGU AMBAYE KILA UCHAO WATU WANAMTAFUTA...YU NDANI MWAKO.....UTATAMBUA KUWA U MWANGAZA.....NA UTATAMBUA JINSI YA KUUTUMIA KUWAMULIKA WENGINE...NA KUIFANYA NURU YA MUNGU ILIYO NDANI MWAKO IONEKANA KWA WENGINE-PONGU JOSEPH

Saturday, January 5

HATUTAMUACHA HATA MMOJA 2013


Tumejifunza mambo mengi kwa mwaka 2012,ambayo yametufanya tutambue sisi ni akina nani na kwa nini tupo hapa duniani.Tumetambua kuwa sisi ndio wasanifu wa maisha yetu wenyewe.Tumejifunza kuwa kila jambo ni jema likitazamwa kwa mfumo chanya na kuwa mambo yote yatokeayo maishani mwetu ni matokeo ya fikra zetu na vitendo vyetu wenyewe...Tumejifunza kuwa upendo ndio silaha ya mafanikio ya kila jambo,upendo ni nuru.tumejifunza pia matokeo yake ambayo ni pamoja na furaha,amani,umoja,uvumilivu na ni mafanikio.Tukajifunza pia kuwa kinyume cha upendo ambayo ni chuki ndiyo matokeo ya maumivu,wivu,visasi,chuki,masengenyo na ndio matokeo ya kila jambo liletalo hasara katika maisha yetu
SISI NI WASANIFU WA MAISHA YETU WENYEWE
 

Leo hii tutajikumbusha kuhusu majukumu yetu …Mwaka mpya ulioanza tuuutazame kwa uchanya wake.Tuanze sasa kutimiza malengo yetu kila mmoja ya kuwepo hapa duniani.Kila mmoja wetu anayo majukumu yake.Kila mmoja ana wito unaomuita ndani mwake,ana sauti ya Mungu ndani yake inayomuita kutenda kwa ajili ya wengine na kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi

Hakuna hata mmoja wetu ambaye hatayapitia magumu,kwa sababu bila magumu kutokea hatuwezi kuendelea.Mwaka huu ni mwaka wa kusonga mbele ...tutasonga mbele,hatutamuacha hata mmoja nyuma
Ni mwaka ambao mwalimu anayeishi katika mazingira magumu yenye milima mingi,ataamka kila siku na kufundisha kwa bidii na kuwanyanyua wengine wengi.Anahitajika huyo ambaye hatalalamika na kusubiri serikali(kwani serikali ni kila mmoja wetu) bali atakuwa ni mfano wa kuigwa wa mbinu bora za kutatua matatizo.Mwalimu popote ulipo amka na kutenda kwa ajili ya wengine.Amka mwalimu.

Sauti ya upendo husikika kwa viumbe vyote.Huu ni mwaka wa kuwa nuru kwa wengine(picha toka helped by animals kwa msaada wa mtandao)


Ni mwaka ambao daktari ataamka mapema na kukumbuka jukumu lake ,ya kuwa hayupo tu kwa ajili ya kutazama idadi ya wagonjwa na kiasi cha fedha,bali yupo kwa ajili ya upendo,akijali utu wa wengine pasipo kubagua hali,kabila,rangi ama hali yeyote na daima atahesabu mafanikio yake kwa kuokoa wengine,kuwainua walio kata tamaa.....na hata akitokea mtoto akaulizwa upendo ni nini,basi amtazame daktari kwa ujasiri akisema......huu ndio upendo.

Ni mwaka ambao kila anayetoa huduma kwa wengine,atatoa akisukumwa na upendo.Kila atazamapo wengine,atambue kuwa anajitazama yeye,na kuwa thamani yake ni thamani ya wengine wote.Anapowatendea wengine akumbuke kuwa anaitendea nafsi yake.Ni mwaka ambao sisi tulio binadamu tutaonesha upendo uliotukuka,utakaofanya nuru ya Mungu iliyo ndani mwetu iwaangaze binadamu engine wasiotambua upendo,ili nao waishi maisha ya upendo.
Sisi ni wamoja,sisi wote ni wana wa Mungu,tofauti zetu zimejengwa na woga ,fikra zetu


Huu ni mwaka ambao tunapaswa kuifanya dunia kuwa sehemu bora,ili nasi tuwe malaika wa dunia hii.

Binafsi jiulize utamtendea nini yule Mungiu ambaye yupo ndani mwako?Je ukiwa katika nyakati za faragha na Muumba wako,utajivunia lipi ulilomtendea?Kumbuka kuwa kama huna malengo ya kutenda jambo lolote huwezi kutimiza lolote.Ni sawa na kusafiri safari isiyojulikana,mahali na hata uelekeo!Tukiweka malengo na kuamini katika kuyatekeleza,hakika yatatimia.

Mimi binafsi najisikia faraja sana kuhamasisha wengine na kuwasaidia wengine waweze kufikia mafanikio HASA PALE WANAPOKUWA NA MSUKUMO UTOKAO NDANI MWAO.Nimejitolea kwa ajiliya wengine na wakati wote najisikia faraja.Ninapokutana na magumu,ninayashinda kwa sababu naamini katika ushindi.Sisi  tumeumbwa kushinda.,na ushindi ni matokeo ya usanifu katika fikra za kila mmoja.

Ninapata faraja ninapoona kuwa yupo nesi ambaye licha ya kwamba anaumwa,anaamka na kwenda kazini kwa ajili ya wengine.Ninafarijika ninapoona kuwa yupo mtu ambaye licha ya kuwa na magumu mengi,anatenda ka ajili ya wengine pasipo kutegemea malipo.Nilikwenda kijijini nilipozaliwa,nikakutana na mama ambaye kipato chake ni kidogo,anaumwa kwa miaka mingi lakini anajitolea chakula na malazi kwa ajili ya wengine....anawafariji wengine,hata anapokuwa katika ugumu sana,hakati tamaa.Maisha yake ni nuru kwa wengi.Daima hamuachi jirani akiwa katika huzuni,nuru yake inaishi.Ni mwanga kwa waliokosa nuru.

Nafarijika kuona wengi ambao wanakwenda mbali na familia zao,mbali na wapendwa wao kwa ajili ya wengine. 
Nafarijika pia kuona wengi ambao wanajinyima kwa ajili ya wengine.Wengi wao wanaishi maisha ya kawaida,(kwa maana ya kipato) lakini wanatambua maana ya thamani yao kwa wengine,wapo tayari kujitolea pasipo kutambuliwa na wengine.Hii inanipa faraja ya kusonga mbele.Hwa wanatambua kuwa sisi binadamu wote ni wamoja ,tofauti zetu ni juu ya fikra zetu wenyewe.

Daima umoja ni nguvu.Usisubiri wengine wachukue hatua.Anza wewe.Mimi nimepata nafasi hii kwa kuandika.Wewe pekeyako pia watosha,unaweza kubadili wengine kwa kusamehe,kuimba,kufundisha,kutoa nakala nyingi za mafunzo kwa wengine,kwa kuwahurumia wengine,kutembelea wagonjwa,yatima,wafungwa na matendo yote yenye kuleta thamani kwa wanaotuzungua.Mwaka 2013 hatutamuacha mtu hata mmoja katika umasikini,chuki,uvivu,visasi,magonjwa huzuni...nk.Mwaka huu hatutamuacha yeyote kwenye giza.Tunao uwezo wa kuyatenda haya yote.Chukua hatua,mabadiliko yanaanza ndani yako.
Wathamini wengine,hata usiowafahamu....

Tujenge mwili mmoja,moyo mmoja na kupambana mpaka mwisho kwa ajili ya dunia iliyo bora na mafanikio kwa ajili yetu na wengine.

kila mmoja wetu anapochukua hatua licha ya vikwazo,tutayafika mafanikio(picha kwa msaada wa mtandao)




Tuishi maisha yetu kwa dhati bila uoga,tuchimbe ndani ya mioyo yetu ambapochemchem ya kila ushindi ipo,Tujifunze thamani yetu ,tuwathamini wengine kwa kuwa wao ni wa thamani kama tulivyo,tusamehe na kutazama mbele,tujali mawazo ya wenginena imani zao tuziheshimu.


Kila mmoja apende nafsi yake,ayapende maisha yake,asanifu vyema vyote vinavyomzunguka,KILA MMOJA AYAFANYE MAISHA YAKE YA THAMANI KWA WENGINE.Tutimize malengo yetu,yanayotokana na sauti iliyopo ndani mwetu,ili ule muda wa kuishi katika dunia hii unapokwisha ,na kifo kukuita,uitike kwa furaha,kwamba uliyaishi vyema,usipate hata sababu ya kuomba upewe tena muda,bali nuru ya maisha yako iwe mfano wa kuigwa milele.Uiage dunia na kuondoka kishujaa,kuelekea katika maisha mengine mapya yenye majukumu mapya.


Tutapita katika magumu mengi lakini daima tutasonga mbele,hatutamuacha yeyote nyuma,tutainuana sisi kwa sisi,hatutatazama nyuma,wala kuogopa kusonga kwa woga wetu,hatutaogopa lolote kwani sisi ni wa thamani,tutakumbuka daima kuwa dunia si sehemu ya ushindani bali ni sehemu ya ushirikiano na umoja na hivyo daima tutafikia tuendako,kwa sababu Mungu yu ndani mwetu.
Ahsanteni sana

Please Give Us Your 1 Minute In Sharing This Post!
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →
Powered By: BloggerYard.Com