Tuanze kwa kutafakari nyakati hizi ambazo hutokea katika maisha yetu mara kadhaa.
kuna nyakati za magumu na upweke ambazo hutufunza |
Ni zile nyakati ambazo unajihisi ukiwa mpweke na kutengwa.Ukihisi ya kuwa hakuna hata mmoja anayekusikilizane. Unapata hisia kuwa upo peke yakojapokuwa wapo watu wengine unaoishi nao na licha ya kuwa unatambua kuwa dunia imejaa watu wengi na viumbe wengi wanaokuzunguka.
Ni kweli kuwa licha ya kuwa dunia imezunguka,ni wewe ndiye uijazayo na unayeisanifu.Wewe kama nafsi watosha.Na unabaki wakati ambao aliyebaki kwako ni Mungu.
Nyakati hizi hutokea pale unapokuwa unajihisi kuwa umekosa kitu(vitu) ulivyovihitaji maishani,na hata wakati kunapohisi kuwa una kila kitu ulichokihitaji maishani mwako.Pia huja katika nyakati ambazo karibu kila kitu ulichokuwa nacho umekipoteza ama umepewa kila kitu ambacho ulikipoteza.
Nyakati hizi zinapofika , ni nyakati za kupona na kuachia majeraha mengi ambayo yalikuwa yakikurudisha nyuma kwa muda mrefu maishani mwako.Na ni nyakati za uvumbuzi wa chemchem ndani mwako.Ni kipindi cha giza kiletacho mwanga.
Na katika nyakati hizi bado kuna kitu muhimu ambacho moyo wako unakihitaji sana na ambacho wengi hukitafuta kwa muda mrefu maishani-Ni kupendwa kwa dhati na kuthaminiwa..
Je kuna yeyote anayenipenda na kunidhamini kwa dhati jinsi nilivyo?.Ni maswali ambayo utajiuliza sana katika nyakati hizi za ugunduzi.
Tumekuwa tukidhani kwamba tunaweza kupata upendo wa dhati na thamani ya kweli toka kwa wengine.Tumetafuta kwa muda sana upendo toka kwa ndugu,marafiki na majirani.Tumetafuta kwa wale tuliowaamini kwa dhati na mara nyingi kuishia kwenye kuumia.
Tukaingia kuutafuta upendo na thamani ndani yetu lakini mara nyingi tumeshindwa kuupata.Hivyo kushindwa kuutambua ndani mwetu kumetupelekea kushindwa kutoa kwa wengine. Na kwa vile tumeshindwa kuupata kwetu tumeitafuta tunapodhani upo ,tunaokosa na kuishia kuogopa kuweka matumaini yetu huko tulipodhani upo.
Na hivyo ndivyo itokeavyo,
Tunatafuta pale ambapo hatukuhifadhi.Na kama hatukuuweka upendo popote vivyo hivyo hatuwezi kuupata.Kile ambacho hatukitoa maishani hatuwezi kukipata kwa sababu hapa duniani sisi ndie wasanifu na wabomoaji.
Kama tunakosa kusamehewa ,ni kwa sababu hatukupata kusamehe.Kama hatuthaminiwi ni kwa sababu hatukupata kuijenga thamani sisi wenyewe.Kama hatuvumiliwi, ni kwa sababu hatukujenga uvumilivu sisi wenyewe.Kama hatupati haki na usawa ni kwa sababu hatukuanza kuijenga ndani mwetu.Kama hatuupati upendo ,basi ni kwa sababu hatukupata kuujenga upendo ndani mwetu. Na kama hakuna ambaye anapata thamani toka kwa wengine,ni kwa sababu hatukuanza sisi kuijenga ndani mwetu.
Mambo yote haya ni lazima yaanze ndani kwetu sisi kisha yaende kwenye maisha ya wengine.
Kwa wengi wetu, tumekosa kujipa thamani yetu sisi na kujipenda , ni havyo ni vigume kutoa kwa wengine.Wengine wengi wanahisi hawana stahili ya mambo yote hayo .Tunajitazama sisi kama dhaifu kuliko wengine ama bora kuliko wengine.
Hatuuoni uzuri uliopo ndani mwetu uliojazwa na uzuri wa Muumba.Hatuoni uaminifu ndani mwetu.Hatuoni usafi ndani mwetu.
Kwa sababu hatuvioni hivi vyote ndani mwetu,hatuwezi kuwapa wengine.
Lakini PIA kwa sababu si kwamba sisi ni vipofu mioyoni mwetu,tunaviona kwa wengine na kuvihitaji tusitambue kuwa tunavyo.Ni mara nyingi tunaona upendo kwa wengine,tunaona huruma kwa wengine,tunauona usafi wa moyo kwa wengine,tunayaona matumaini kwa wengine. Hivyo kwa kuviona kwa wengine, tunajaribu kutenda kwa baadhi yao lakini si ndani mwetu
mara nyingi tunaona upendo,huruma kwa wengine |
Je tunaweza kujitendea nafsii zetu?
Mara nyingi tunashindwa kwa sababu ya vidonda tulivyonavyo.
Kwa sababu ya vidonda tulivyonavyo,tunashindwa pia kutibu majeraha ya wengine.Hivyo hatuthamini jinsi dunia inavyotuhitaji kila mmoja kwa nafsi yetu.
Tunashindwa kutambua kuwa dunia inahitaji kile kitokacho ndani mwetu ikiwemo upendo,usawa,haki,thamani kwa wengine,uvumilivu na kujitolea.Tunaishia kuilamu dunia tusijue kuwa ni sisi ndio tulioanza kuisanifu.Na hivyo tunaweka picha ndani mwetu kuwa dunia ni mbaya na onevu tena sehemu ya kupita kwa machungu.
Hatuwezi kupata kutoka katika dunia vile ambavyo hatukuvipanda. Na sasa tunapaswa kukumbuka hapa kuwa : Chochote ambacho hatukukipanda duniani,hatuwezi kukipata katika dunia hiyohiyo.Tunavuna tulichopanda
Hapa ndipo unapokuja wakati tunapogundua kuwa sisi ndio wasanifu wa dunia na kila kilichomo.Ni wasanifu wa maisha ya leo na ya kizazi kijacho.Hakuna atakaye tupatia chochote kile ambacho hatukuanza sisi kukipanda na kukitoa kwa dunia hii tuishimo.Na mara nyingi tunamuomba Mungu na wakati mwingine kumlaumu kwa kutotupatia kileambacho hatukuanza sisi kukitengeneza na hata kukitoa kwa wengine pale tulipostahili kufanya hivyo
Nadhani ni wakati kwa viongozi wetu wa dini kuanza kufundisha hili.
Tunaweza kuanza kuona mifano katika kati mahusiano yetu.Kama huwezi kumsamehe unayeishi nae,unashindwa kumpenda,kuishi nae kwa amani na uhuru na hata kumvumilia,ni vigumu kutarajia kupata kutoka kwa huyohuyo unayeishi nae na kulala upendo,thamani,uvumilivu,uhuru,amani na thamani ya kweli.Tutapata kadiri tulivyotoa
Huwa tunafikiri kuwa ndani ya mahusiano,mwenzi atakupatia vitu ambavyo unajihisi huna.Tunadhani tutapata upendo ambao sisis hatuutoi,msamaha ambao sisi wenyewe hatuutoi.Ni huu ni moja ya uongo mkubwa tunaoajidanganya ndani ya nafsi zetu.
Tunapotamani kupatiwa pasipo kutoa,mwisho wake kila kitu hufifia,kasha chuki huingia na kasha mahusiano hufa.Kisha tunagundua kuwa ni sisi wenyewe tulijidanganya.Sasa tiunatambua kuwa hakuna pa kukimbilia zaidi ya Mungu. Tunarudi kwa Mungu na kumwambia…"Tafadhali Mungu wangu naomba unisamehe.Naomba unijalie amani na upendo,nijalie uvumilivu na moyo wa kujitolea.Nakuomba baba unijalie hivi nami niwagawie wenzangu."
Kwa sasa dunia ipo kwenye machafuko na chuki. Majivuno,visasi na dharau vimetawala.Tumejenga wenyewe tena toka ndani mwetu.Na muda si mrefu baada ya mambo haya kukithiri,Binadamu watatambua kuwa sasa tutavipata kwa Mungu,naye ni Muweza na chemchem ya kila kitu.
Na wakati huo binadamu watatambua kuwa hakuna utengano kati ya Muumba,chemchem ya kila jambo na Nafsi ya kila binadamu.Binadamu watatambua kuwa miili yetu imebeba nafsi ndani,ambapo ndiko hekalu la chemchem ya kila jambo huishi. Kila mmoja atatambua umuhimu wa nafsi yake na jinsi anavyohusika katika ujenzi wa dunia.Kila mmoja ataanza kuchukua hatua katika kutambua matokeo ya kila jambo analotenda.
Kila nafsi itajifunza kupanda na kutaraji mavuno.Kila nafsi itathamini nafsi nyingine na kila nafsi itatambua kuwa inahusika kujenga dunia mpya na haitakuwa tayari kulaumu dunia na kudai dunia kile ambacho haikukipanda wala kukitoa.Kisha dunia itakuwa sehemu bora ya kuishi
Ndani mwako kuna pumziko la kweli,furaha,amani,nuru ya kweli na chemchem ya uumbaji wa Mungu ambayo Mungu amekupa na kukuleta hapa duniani.Ukisikiliza moyo wako unaweza kutambua mengi yaliyo ndani mwako....Kazi yako ukiwa hapa duniani ni kutoa ulichonacho,kilicho ndani mwako kwa ajili ya wengine
Mpaka sasa wachache wanalitambua hili.Na wasiotambua huilamu dunia kila kukicha.Na hivyo wasio tayari kutambua hili watasubiri mpaka ule wakati watakapolia na kugundua hakuna zaidi ya Mungu na kasha kugundua hekalu la chemchem yake ndani mwao . Hii itakuja bada ya kubomoa mengi…ndoa,familia,amani,upendo na kIsha nafsi NA baadae kufanya juhudi kujijenga upya
Kila mmoja akiwa kama nafsi huru anapaswa kuchukua hatua,hasa kutambua kuwa hakuna mwingine zaidi ya Mungu, na kasha kuchimba ndani kutambua kuwa sisi ni hekalu iishipo nuru na chemchem ya kila tunachokihitaji
Unapoanza kumuona Mungu katika kila kiumbe kinachokuzunguka unatambua kuwa sasa umezaliwa upya.Sauti yake inakuwa ikiongea nawe ndani mwako toka ndani yako.Unatambua kuwa Mungu hayupo mbali nawe bali yupo ndani mwako wakati wote.Unaruhusu nguvu na chemchem ya kila ushindi kufanya kazi ndani yako na kukupa nafasi ya kugundua nguvu hii iliyo ndani mwako na kuitumia kuifanya dunia kuwa sehemu bora kwa viumbe wote
.Mungu ametupatia uwezo mkubwa wa kuyafanya maisha yetu kuwa yenye faida kwa wengine,na husubiri maamuzi yetu ili kutuonesha njia.Tunapokuwa tayari anatufundisha maana ya kuwa hapa na thamani ya maisha yetu . Ndipo unapomjua tena si kama kiumbe cha kutisha ama kisichoonekana lakini kama sehemu muhimu ndani mwako.Kisichoonekana ndani mwetu kinazaliwa upya na kuonekana kwa kila anayekuzunguka.Kisha hutupatia kila uwezo na kuingia ndani ya kila kilicho mwilini mwetu kwa maelfu,tayari kwa kumtumikia kwa njia mbalimbali. Tunajenga dunia mpya yenye matumaini na furaha