Tuachane Na Fikra Za Malalamiko, Upanuliwe Wigo Katika Ubunifu
Na: Meshack Maganga, Mjengwablog-Iringa.
Rais
wa enzi hizo wa taifa la Marekani Theodore Roosevelt (Oktoba 27, 1858-
Januari 6, 1919) alipata kusema, “What we need is more people who
specialize in the impossible”, kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili ni
kwamba, “Tunachohitaji ni watu wengi zaidi ambao wamebobea katika
kufanya mambo yanayoonekana ama kudhaniwa kuwa hayawezekani,
(specialists)”.
Kauli
ya Roosevelt inanikumbusha habari ya vijana wawili waliohitimu Chuo
Kikuu Cha Dar es Salaam. Vijana hawa walipokuwa chuoni muhula wa pili,
mwaka wao wa kwanza wa masomo walibuni biashara ya usafiri wa bajaji.
Walichanga shilingi laki nane kutoka fedha ya mkopo wanayopewa na bodi
ya mikopo ya elimu ya juu, ndipo wakanunua gari hiyo ya miguu mitatu na
kufanya biashara hiyo ambayo iliwasaidia sana kuwakwamua kiuchumi.
Kwa
mujibu wa maelezo yao ni kuwa wakati wakitambulisha wazo lao kwa wenzao
waliambiwa “hilo haliwezekani!”. Wanasema kuwa katika kauli ambayo
hawataisahau ni ile waliyoambiwa hivi, “Hiki kitabu cha UDSM kitawapaje
muda wa kusimamia hiyo biashara yenu? Labda kama mpo tayari kwa supp
zisizokwisha zitakazofuatiwa na disco”. Maneno hayo hayakuwazuia,
walianzisha biashara wakaendeleza na bado walifaulu masomo yao.
Wakafanikisha kisichowezekana!
Miaka
ya karibuni watanzania tumeshuhudia kuanzishwa kwa utaratibu wa
kuchangia gharama katika elimu ya juu. Suala hili ndilo lililopelekea
kuundwa kwa bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Bodi hii hutoa
mikopo kwa wanafunzi hao; katika viwango tofauti tofauti kutegemea na
vigezo ambavyo imeweka kwa mujibu wa sheria na taratibu za uendeshaji wa
bodi hiyo.
Mabadiliko
ya mifumo ya gharama za elimu ya juu nchini Tanzania yanatupa somo
muhimu sana kuhusu alama za nyakati. Ni suala la uhakika kuwa siku
zijazo mchango wa moja kwa moja wa serikali katika kusomesha vijana wetu
utafutika. Hapa naikumbuka kauli aliyopata kuisema Mkurugenzi wa shule
ya Star International ya mjini Iringa, Madam Jessca, namnukuu,
“Ninawekeza leo kwa kutoa sadaka na kuimarisha biashara zangu, ili siku
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itakapokosekana, wanangu
wasishindwe kupata elimu ya juu” mwisho wa kunukuu. Hakuna haja ya
kupambana na nyakati kwa kuzililia zama za Mwalimu J.K Nyerere ambapo
elimu ilitolewa bure, bali tukabili nyakati zilizopo na kujipanga kwa
nyakati zijazo
Tangu
kuundwa kwa bodi hii kumekuwepo na malalamiko mengi sana kutoka kwa
wadau mbalimbali kuhusiana na mfumo huu wa uchangiaji wa gharama pamoja
na utaratibu na utendaji wa bodi hii katika kufanikisha lengo hili.
Kuna
wadau ambao kwa asilimia mia moja wanapingana na utaratibu huu wa
kuchangia elimu ya juu na kuna kundi ambalo linaunga mkono. Sehemu kubwa
ya kundi la pili inakwazwa na namna bodi hii inavyotenda kazi zake na
kupelekea, mikopo kuchelewa kuwafikia wanafunzi kwa wakati husika,
kukosekana kwa mbinu sahihi katika kubaini wapi wanastahili madaraja
gani, pamoja na upendeleo (ama uzembe?) katika kupanga madaraja haya ya
mikopo.
Bodi
hii hutoa mikopo kwa madaraja kwa upande wa ada, “tuition fees” pamoja
na fedha ya mafunzo kwa vitendo. Kuhusu fedha za chakula na malazi
wanafunzi hupewa kiwango kinacholingana bila kuzingatia madaraja
waliyopata. Hadi wakati huu bodi hii inatoa shilingi, elfu tano kwa
siku, ama laki moja na nusu kwa mwezi, kama gharama za chakula na
malazi.
Kumekuwa
na changamoto zinazobainishwa na wanafunzi hawa kwamba kiwango cha
fedha wanazopewa hazitoshi katika kuwawezesha kusoma kwa uzuri. Ingawaje
vyuo hivi vipo katika maeneo tofauti tofauti, changamoto zinazowakabili
wanafunzi hawa nyingi zinashabihiana.
Wanafunzi
wengi wanatoka katika familia za kimasikini ambazo pengine hata
70,000/= ya kulipia ada katika sekondari walizotoka zilikuwa zinawapiga
chenga. Sasa chukulia kuwa huyu mwanafunzi anapewa mkopo wa asilimia
themanini, na yupo katika chuo ambacho gharama ya shahada ya kwanza kwa
mwaka wa masomo ni 1,800,000/= Hii ina maana kuwa bodi ya mikopo
itamlipia ada shilingi milioni moja na laki mbili na itampa shilingi
milioni moja na laki mbili ya malazi na chakula kwa mwaka.
Katika
ada atakuwa anadaiwa shilingi laki sita, (600,000/=). Hizi laki sita
anatakiwa azilipe kutoka katika ile fedha ya malazi na chakula. Akilipa
hizo ina maana anabakiwa na shilingi laki sita tu kwa mwaka wa masomo.
(Isisahaulike kuwa bodi ina ukomo wa viwango vya kuwalipia ada wanafunzi
inaowadhamini, ukomo huo ni milioni moja na nusu kwa mwaka wa masomo.)
Laki sita kwa miezi nane ya masomo, kulipia pango, kununua chakula na
kujipatia mahitaji mengine ya msingi kiuhalisia haitoshi.
Tatizo
la mikopo isiyotosha elimu ya juu ni la kimtambuka kwa maana kuwa
linahusisha pembe nyingi. Kuna suala la ada kubwa katika baadhi ya vyuo,
kiwango kisichotosheleza cha fedha inayotolewa na Bodi ya mikopo kwa
siku kwa chakula na mavazi, mfumo wa utoaji wa elimu ya juu nchini
pamoja na fikra zilizopo miongoni mwa wanafunzi wengi wanaosoma elimu za
juu.
Mwanazuoni
mmoja wa nchi za Magharibi, G.K Chesterton amewahi kuelezea shida
inayowakumba watu kupata ufumbuzi kwa matatizo yanayowakabili, yeye
anasema “It isn’t that they cant see the solution. It is that they can’t
see the problem” (Sio kwamba hawaoni ufumbuzi wa tatizo, ila ni kuwa
hawalioni tatizo). Kuwa na tatizo ni kitu kimoja na kulielewa tatizo
(chanzo cha tatizo, lilipo na madhara yake ikiwa halitatatuliwa) ni kitu
cha pili. Tuna tatizo la mikopo isiyotosheleza kwa wanafunzi wa elimu
ya juu lakini ufumbuzi wake umeendelea kuwa suala la kufikirika na
imebaki kulaumiana.
Wanafunzi
wa elimu ya juu na baadhi ya wadau wanadhani kuwa suluhisho la tatizo
hili ni kuongezwa kwa kiwango cha mikopo. Serikali inasikia lakini
haitendi kwa mujibu wa matakwa haya. Tayari pande mbili husika
hazijakubaliana na ufumbuzi wa tatizo hili; ina maana kuwa eidha upande
mmoja haujalielewa tatizo vizuri ama pande zote hazijalielewa.
Hata
hivyo mwathirika mkubwa ni huyu mwanafunzi anayesomeshwa na bodi ya
mikopo katika taasisi hizi.Hakuna namna zaidi ya mwanafunzi huyu kupanua
wigo wa fikra zake na kuona ni namna gani ataishinda changamoto hii kwa
mbinu na njia zilizo halali. Daima ufahamu uliopanuliwa katika njia
mpya za kupata majibu ya changamoto, haurudi kamwe katika mipaka yake ya
mwanzo. Zikomeshwe fikra za malalamiko, wigo upanuliwe katika ubunifu,
badala ya mawazo ya kuilaani Bodi ya mikopo na serikali kwa mikopo
isiyotosheleza ni vema kupanua fikra katika kujitegemea
Huu
ni wakati ambao vijana wetu wanatakiwa kushusha chini vidole vyao
vilivyoielekea serikali na kutazama ni nini kinaweza kufanyika
kujikwamua. Mwanaharakati wa kweli hupambana kwa ajili yake na kwa ajili
ya vizazi vyake vijavyo. Tujiulize, maswali yafuatayo. Je, vizazi
vijavyo vitaishije pindi mchango wa serikali kwa elimu zao
utakapofutika, ikiwa hatuweki misingi ya kujitegemea sasa? Vilio vyetu
vimesikilizwa kwa kiasi gani? Je, tuendelee kulia ama tufute machozi,
tujifunge mikanda tutazame tatizo kwa namna tofauti?
Hakuna
maana ya kuweka nadhiri za chuki zitakazoliangamiza taifa kutokana na
yale yanayopitiwa kwa sasa. Nafahamu wapo vijana wetu ambao kutokana na
adha wanazozipata katika utaratibu huu wa mikopo, wananadhiri kuja
kulipiza kisasi. Nao wanaweka nia za kuja kupukutisha rasilimali za
taifa ili kunufaisha matumbo yao na ya ndugu zao. Vijana wetu wa vyuo
vikuu lazima watambue jambo hili, ya kuwa uovu wa baadhi ya viongozi
waliopo madarakani haupaswi kuhalalisha wengine kutenda maovu. Msomi ni
lazima awe na ndoto za kuubadili ulimwengu wake kutoka hatua moja kwenda
nyingine iliyobora zaidi.
Ipo
haja kubwa sana kwa wanafunzi wa elimu ya juu kujijengea utamaduni wa
kijasiriamali ili kwa fedha kidogo wanayokopeshwa waweze kuzalisha na
kufidia upungufu unaojitokeza katika gharama za masomo yao. Nikigusia
suala la ujasiriamali inawezekana kuwepo na vikwazo vingi, ikiwemo muda
na mazingira ya kufanya huo ujasiriamali, ukosefu wa rasilimali (mitaji)
na mengine mengi upendayo kuorodhesha. Anayevuka na kutatua vikwazo
hivyo, huyo ndiye “specialist” wa yasiyowezekana!
Wanafunzi
wengi waliopo katika taasisi zetu si wenye juhudi katika kufikiria,
ubunifu na kufanya kazi kwa kujituma. Waangalie wanafunzi hawa jinsi
wanavyoutumia muda wa likizo zao ndefu na fupi, mara nyingi hawafanyi
kazi eidha za kulipwa ama za kujitolea. Mara nyingi hutoa sababu
zinazosema na kuonesha kuwa hakuna kazi. Wananata, hawataki kukaa
vijijini hata kama kuna fursa nyingi, wanataka kumalizia likizo zao Dar
es Salaam.
Kuna
wakati unaweza kudhani kuwa vyuo vya elimu ya juu hupendelea kufanya
udahiri wa kimikoa, kwa sababu wengi wanataka kutambulika kama wakazi
wa majiji hasa Dar es Salaam. Miezi mitatu ama mine ya likizo mtu yupo
jijini kwa mjomba, binamu au kwa wa kutoka kijiji kimoja kule Songea,
hana kazi zaidi ya kula, kulala, kuoga na kuangalia TV. Wakati mwingine
analala sebuleni, na kulala kwake ni mpaka wote waende kulala! Kama
mwanafunzi huyu angeenda hata kijijini kwenye kata ya nyumbani kwao
akajitolea kufundisha shule ya kata kwa miezi minne angekuwa amezalisha
angalau laki mbili!
Ninao
mfano wa rafiki yangu mmoja ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha
Mzumbe, ambaye amekuwa mbunifu na alishaupiga teke ulimbukeni wa kujiona
kuwa eti “wa elimu ya juu” kuna kazi hatakiwi kuzifanya hata kama
zinamwingizia kipato. Huyu kila likizo huwa anarudi kijijini kwao na
huko huutumia muda wote katika kufanya biashara ya alizeti. Huzunguka
vijiji mbalimbali akikusanya na kisha kusafirisha alizeti hizo kwenda
mjini. Katika moja ya likizo yake ya miezi minne, aliingiza mtaji wa
shilingi laki tatu (fedha za bodi ya mikopo) na kuzalisha jumla ya
shilingi milioni moja na laki sita.
Hawa
wanafunzi wa vyuo vya juu, imewapasa kuwa na macho ya ndani yenye uwezo
wa kuvumbua na kuzitumia fursa. Kuna kuwekeza kwa aina nyingi ambako
wakati mwingine mtu si lazima awepo muda wote katika kusimamia
alivyowekeza. Inawezekana kumiliki hisa katika makampuni, kuingia
ushirika wa kibiashara (partnership) ama kuitumia jamii ya wanafunzi
wanaowazunguka, kubuni biashara ama miradi itakayowaingizia vipato.
Pale
juu katika makala haya nilitaja pembe zinazochangia mtambuka wa tatizo
hili. Ingawa niliacha pembe zingine tatu, ni dhahiri kuwa zinachangia
sana katika kufanikisha ufunguzi wa hizi fikra za hawa wanafunzi wa
elimu ya juu. Nitachambua pembe hizi katika makala mengine, lakini
itoshe tu kusema, ukiwa na tatizo ni lazima ujikague na kujirekebisha
vizuri kabla hujamvaa anaechangia kukua kwa tatizo lako.
Leo
hata kama wanafunzi hawa wakaongezewa fedha na kulipwa 20000/= kwa
siku, bado watagundua kuwa fedha hiyo haiwatoshi. Suluhisho sio kuililia
serikali pekee wakati tumekaa na kubweteka. Tutalala, tutaamka,
tutaandamana na kujikuta bado tuko pale pale. Badala ya kuwaza ukahaba,
wizi na ujanja ujanja wa kukopeshana na kudhulumiana hebu wasomi wetu
waanze kutumia taalveuma zao kufanya ubunifu na kujikwamua. Hii
inawezekana ila kwa wale watakaojitolea ku-specialize katika
yasiyowezekana.
Na kila mwanafunzi wa elimu ya juu anayeguswa na hili analazimika kuwa specialist wa yasiyowezekana!
Je! Unahitaji mkopo wa haraka ili uondole deni lako au unahitaji mkopo wa usawa ili kuboresha biashara yako? Umekataliwa na mabenki na mashirika mengine ya kifedha? Je! Unahitaji uimarishaji wa mkopo au mikopo? Utafute tena kama tuko hapa kufanya matatizo yako yote ya kifedha kitu cha zamani.
ReplyDeleteHii ni kampuni rahisi ya mkopo. Tunatoa mikopo kwa wale wanaopenda kiwango cha riba cha 2%. Mipangilio mbalimbali kutoka $ 5,000.00 hadi dola za dola 100,000,000.00.
Mikopo yetu ni bima nzuri kama usalama wa juu ni kipaumbele chetu.
Wasiliana nasi kwa barua pepe: oceanfmortgages@gmail.com
Uzidi
Max Bent
oceanfmortgages@gmail.com
Mikopo ya 2% ya awali na dhamana
oceanfmortgages@gmail.com